"Sihitaji msaada wa kifedha!" Mumewe Zari, Shakib Cham akanusha kuomba pesa

Shakib amewaonya watu dhidi ya kutuma pesa zozote kwa yeyote anayedai kuwa yeye au mwakilishi wake.

Muhtasari

•Shakib alibainisha kuna watu wanaodai kuwa yeye au wawakilishi wake ambao wamekuwa wakiwalaghai wanamtandao kwa kuwaomba watume pesa.

•"Kuwa mwangalifu na usichangie au kutuma pesa kwa mtu yeyote anayedai kumwakilisha," akaongeza.

Image: INSTAGRAM

Mfanyibiashara maarufu wa Uganda, Shakib Cham Lutaaya amewaonya watu dhidi ya kuingia katika mtego wa matapeli wanaolenga kuwaibia pesa kwa kutumia jina lake.

Katika taarifa kwa mashabiki wake siku ya Jumatatu, mume huyo wa sosholaiti Zari Hassan alibainisha kuwa kuna watu wanaodai kuwa yeye au wawakilishi wake ambao wamekuwa wakiwalaghai wanamtandao kwa kuwaomba watume pesa.

Shakib hata hivyo aliweka wazi kuwa hahitaji msaada wa pesa kutoka kwa mtu yeyote na akawaonya watu dhidi ya kutuma pesa zozote kwa yeyote anayedai kuwa yeye au mwakilishi wake.

“Taarifa muhimu! Tafadhali fahamu kuwa Shakib Cham hahitaji usaidizi wa kifedha kutoka kwa mtu yeyote. Kunaweza kuwa na kurasa bandia au watu binafsi wanaodai kuwa Shakib Cham au wawakilishi wake wanaomba pesa. Usiwe mwathirika wa ulaghai huu!” Alisema Shakib kupitia mitandao ya kijamii.

"Kuwa mwangalifu na usichangie au kutuma pesa kwa mtu yeyote anayedai kumwakilisha," akaongeza.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya  Zari Hassan kumkosoa hadharani mwanaume huyo wa miaka 32 na kumshutumu kwa kutoleta chochote katika ndoa yao.

Mapema mwezi huu, sosholaiti huyo alizamia kwenye mitandao ya kijamii kumzomea mumewe Shakib na kutishia kumuacha.

Katika kipindi cha moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa mumewe hana uhakika kuhusu ndoa yao na amekuwa akihoji uhusiano kati yake na mzazi mwenzake, Diamond Platnumz.

Zari alisema alilazimika kufanya kipindi cha moja kwa moja ili kueleza wazi kuwa yeye na Diamond hawako kwenye uhusiano wowote wa kimapenzi, ili tu kumhakikishia mumewe kuhusu auaminifu wake katika ndoa yao

“Ngoja niwaambie kitu, Nikitaka kumrudia Diamond naweza kurudi. Ikiwa Diamond anataka kunirudia, anaweza kurudi. Lakini sisi tumemalizana. Sisi tumemalizana kabisa. Simtaki, hanitaki,” Zari alisema Jumapili usiku.

Sosholaiti huyo aliweka wazi kuwa ana mume na mzazi mwenzake pia ana mpenzi.

“Mume wangu hajiamini sana, na hilo linaleta matatizo mengi. Lazima niwe hapa kuelezea. Kweli? Boss lady mzima, inabidi nifanye kipindi chote cha moja kwa moja, ili tu kuthibitisha uhakika kwa mume wangu. Kipindi hiki ni kuthibitisha kitu kwa mume wangu,” aliongeza.

Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 43 alibainisha kuwa ana sifa zote nzuri na anaweza kuwa na mtu yeyote ambaye anataka kuwa naye.

"Lakini nilimchagua mume wangu, na sijali jinsi nyinyi mnamwona. Ooh, amefilisika, hafai vya kutosha, sijali. Nilimchagua. Nilichagua kuwa naye kama mume wangu, kisha ananiweka katika hili!!,” alisema.

Zari alidokeza kuwa mumewe hana budi kuacha kutokuwa na uhakika kuhusu ndoa yao ikiwa anataka iendelee vyema.