Mchekeshaji maarufu wa Kenya Mammito Eunice anatarajia mtoto wake wa kwanza hivi karibuni.
Mchekeshaji huyo wa zamani wa kipindi cha Churchill Show alitangaza habari za ujauzito wake siku ya Jumanne katika video ya kibunifu ambayo aliichapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Katika video hiyo, mrembo huyo mcheshi alionekana akicheza na mpira wa kandanda kwenye uwanja usio na watu kabla ya kufichua ujauzito wake mzito.
“Kwani unataka nishike mipira ngapi? Je, moja haitoshi?" Mamito alisema baada ya kuonyesha ujauzito wake.
Aliendelea kueleza kuwa ujauzito ni baraka na anaukubali.
“Mimba
ni baraka *2. Mimi Mammito, tulipatana na Pappito, tukatengeneza kapappito,”
alisema.
Katika chapisho lingine, Mamitto alitoa shukrani zake za dhati kwa mashabiki wake wengi ambao walikuwa wamempongeza kwa hatua kubwa ya maisha ambayo amepiga.
Pia alielezea shauku yake ya kuingia katika uzazi na kukutana na mtoto wake wa kwanza.
“Asanteni kwa jumbe nzuri za pongezi. Ninashukuru kwa safari mpya ya #babyto baking,” alisema.
"Moyo wangu umejaa .. siwezi kusubiri kukutana nawe," aliongeza, akimzungumzia mtoto wake ambaye hajazaliwa.
Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show hata hivyo hakufichua maelezo zaidi kuhusu ujauzito wake. Mpenzi wake, ambaye pia anakusudiwa kuwa mzazi mwenzake pia amebaki kuwa kitendawili.
Wanamitandao wengi, wakiwemo mastaa wenzake wameendelea kumsherehekea na kumtakia kila la heri katika safari yake ya ujauzito na uzazi.
Habari kuhusu ujauzito wa Mammito zilikuja siku moja tu baada ya yeye kudai kuwa hajashiriki katika tendo la ndoa mwaka mzima huu.
"Nimekuwa bila mapenzi mwaka huu, na hilo limenifanya kujiangazia sana," alidai siku ya Jumatatu.
Wanamitandao kadhaa hata hivyo walikuwa tayari wameibua shaka kuhusu madai yake huku wengine wakidokeza kuwa alikuwa anatarajia mtoto.