Msanii na mfanyibiashara KRG the Don ametangaza marufuku kwa marafiki na wanafamilia wake ambao wana mazoea ya kutumia pikipiki katika usafiri wao.
Akieleza sababu ya kuwapiga marufuku wanafamilia na marafiki kutumia pikipiki, KRG alifichua kwamba ndugu yake alihusika katika ajali mbaya, jambo lililomuacha katika mshtuko mkubwa.
“Leo nilipitia moja ya siku ndefu zaidi katika maisha yangu, nilikuwa nusra nimpoteze kaka yangu wa damu kwenye ajali ya barabarani ikihusisha pikipiki na gari huko Kiambu. Kusema kweli sijawahi paniki jinsi ambavy nilipaniki leo,’ KRG alisema.
Hata hivyo, msanii huyo alifichua kwamba kaka yake kwa sasa anaendelea vizuri japo aliata kuvunjika mkono wake wa kulia.
Alitumia fursa hiyo kutoa neno la ushauri kwa waendesha pikipiki kuhusu usalama wa barabarani.
“Tunamshukuru Mungu kwa sasa yuko nje ya hatari japo alivunjika mkono wake wa kulia na mguu. Nyinyi waendesha pikipiki wote hakikisheni muda wote mmevalia ifaavyo. Mnaweza kuwa si yeye mko katika njia mbaya lakini ni watumizi wengine wa barabarani wanaowafanyia vibaya.”
Kutokana na hilo, mfanyibiashara huyo alisema atakuwa na ugomvi usioisha na marafiki na wanafamilia wake ambao atawakuta wakitumia pikipiki.
Alitishia hata kuchoma pikipiki hizo pindi atakapowakuta wanafamilia na marafiki zake wa karibu wakizitumia kwa usafiri.
“Kuanzia leo hadi siku ya mwisho ya maisha yangu, kama nitawapata wanafamilia wangu au hata marafiki zangu wa karibu kwenye pikipiki, jua tu kwamba tutapigana vita naapa kwa Mungu. Zaidi ya hapo nitaichoma pikipiki hiyo hapo ukiangalia, mnipeleke polisi tu,’ alisema.