Mchungaji Robert Burale amefichua kwamba amepitia
mapito mengi sana katika mitandao ya kijamii, yote yakilenga jinsi anavyojibeba.
Akizungumza kwenye podikasti ya Lessons At 30 na
mkuza maudhui maarufu, Dr Ofweneke, Burale alisema kwamba ilimchukua kipindi
cha miaka 3 kuwa na ukakamavu wa kutobebwa na kauli hasi za watumizi wa
mitandao ya kijamii.
“Ilinichukua
miaka 3 kuwa mkakamavu kwa maoni hasi mtandaoni. Maoni mabaya zaidi nimewahi
kuyaona kuhusu mimi, siwezi hata weka kidole kwayo lakini kwa wakati Fulani kuna
mtu alijaribu kumshambulia binti yangu.”
“Nilimwambia
mtu huyo kwamba sitomuendea nikiwa kama Pastor Burale bali ningemwendea kama
Robert na aliomba msamaha,’ Burale alisema.
Alifichua kwamba kuna baadhi wamekuwa wakijaribu
kumshambulia kutokana na chaguo la rangi ya mavazi yake muda wote.
Burale alifichua kwamba aliwahi itwa mchungaji wa
iluminati kutokana na upendo wake kwa mavazi ya rangi nyeusi.
“Wenye
chuki hawawezi kusema chochote cha hakika, kuna mtu aliniita pasta wa iluminati
eti ndio maana nahubiri nikiwa nimevaa nguo nyeusi. Ukweli ni kwamba mimi
napenda nguo nyeusi na nitaendelea kuvaa nguo nyeusi. Mimi navaa suti nyeusi na
hata boxer nyeusi, ni vile tu siwezi onyesha,”
Burale alisema.
Burale alisema kwamba matukio kama hayo yamemfanya
kubana idadi ya marafiki zake, akisema kuwa yeye ana marafiki 4 tu.
“Babangu
alikuwa anatumia vitabu viwili kunifunza; Biblia na kitabu cha Shakespear. Aliniambia
kwamba mwanangu usiwe na marafiki wengi. Kuwa mkarimu kwa kila mtu lakini
usikuwe rafiki wa kila mtu. Kusema kweli mimi huwaambia watu kama uko na
marafiki zaidi ya 5 unafaa kuenda kukaguliwa kichwa chako. Mimi marafiki zangu
wakienda sana ni 4,” Burale alisema.
Mchungaji huyo alisema kuwa marafiki katika mzunguko
wa maisha yake ni wa kategoria nne; marafiki wa maeneo ya kuegesha gari,
marafiki wa sebuleni, marafiki wa jikoni na mawafiki wa chumbani.
“Mimi huwa makini sana kuhusu ni nani ninakubalia
kuingia katika nafasi yangu. Ndio maana nasema kuna marafiki wa maegesho ya
magari, kuna marafiki wa sebuleni, kuna marafiki wa jikoni na kuna marafiki wa
chumbani.”
“Marafiki
wa maegesho ya magari ni wale ambao mnaweza jadili kitu chochote huko nje,
marafiki wa sebuleni ni wale ambao unakubali kuingia kwako na muwe na
mazungumzo ya kina na hata kutoka kwenye ziara nao, marafiki wa jikoni ni wale
unaweza kuamini kwa sababu jikoni kuna kisu, watu ambao hawawezi kukuchoma
mgongoni na marafiki wa chumbani ni wale ambao unaweza ukaamini na siri zako za
ndani ambazo zinaweza kufanya kuwa mdhaifu lakini hawawezi kukuabisha,”
mchungaji huyo alisema.