BILIONEA Elon Musk amezua mjadala kwa tweet ya hivi majuzi
inayopendekeza kwamba jamii inapaswa kufundisha hofu ya kutokuwa na watoto
badala ya hofu ya ujauzito.
Maoni hayo yamepata kuungwa mkono na kukosolewa kwa mizani
sawia, na kuchangia katika majadiliano yanayoendelea kuhusu kupungua kwa
viwango vya kuzaliwa na maoni ya Musk kuhusu masuala ya idadi ya watu.
Musk, ambaye hivi karibuni alikua baba kwa mara ya kumi na
mbili mapema mwaka huu, amekuwa akielezea wasiwasi wake juu ya upungufu wa watu
duniani.
Anaamini kuwa kuhimiza watu, hasa wale walio na IQ ya juu,
kuwa na watoto wengi ni muhimu kwa mustakabali wa ustaarabu. Familia kubwa ya
Musk inasisitiza kujitolea kwake kwa imani hii.
Katika chapisho lenye kuchochea fikira kwenye X, Musk
alipendekeza mabadiliko ya dhana, akiwahimiza watu waachane na kupandikiza hofu
ya kupata mimba na, badala yake wazingatie hofu ya kile ambacho kingekuja
katika ulimwengu usio na mimba au mimba kidogo—kutopata mtoto.
Chapisho hilo limeibua vifijo na ukosoaji, na kuibua
mijadala kuhusu viwango vya kuzaliwa duniani, ambayo inapungua kwa kasi katika
nchi zilizoendelea.
Hii inasababisha ukosefu wa wafanyakazi kutokana na idadi ya
watu kuzeeka.
"Badala ya kufundisha hofu ya ujauzito, tunapaswa
kufundisha hofu ya kutokuwa na watoto", Musk alisema akijibu chapisho la X
ambalo lilionyesha kuwa viwango vya kuzaliwa nchini Uswidi na Uingereza viko
katika viwango vya chini zaidi.
Katika baadhi ya nchi zinazoendelea au zenye kipato cha
chini, kiwango cha kuzaliwa kinaongezeka kwa kasi, na hivyo kuweka shinikizo
kwa rasilimali chache zenye uwezo wa kutumbukia katika janga la kibinadamu na
ukosefu mkubwa wa ajira.
Matamshi ya bilionea huyo yanayopendekeza kwamba viwango vya
chini vya uzazi vinavyozikumba nchi za Magharibi vinatokana na uadui wa
kitamaduni dhidi ya ujauzito na ulezi wa watoto maoni aliyotoa wakati wa
mahojiano na mchambuzi wa kihafidhina Tucker Carlson mwezi uliopita.
"Tunahitaji kuacha kuwaogopesha wanawake kwamba kuwa na
mtoto kunaharibu maisha yako," alisema.
“Huu ni uongo. Tunawatia hofu wasichana kwa kusema kwamba
ukipata mimba, maisha yako yamekwisha. Hivi ndivyo shule zinavyofundisha.”
Ingawa Musk alikubali kwamba mimba za utotoni ni tatizo kwa
jamii ya Marekani, alitambua kuwa na mtoto kama “mojawapo ya mambo ya
kufurahisha zaidi na yenye kuleta furaha unayoweza kufanya.”
Alihusisha juhudi za kuwashawishi Waamerika wasiwe na watoto
kwa toleo "lililokithiri" la "harakati za mazingira."