ALIYEKUWA msanii wa miziki ya kidunia, Kush Tracey
hatimaye amempokea roho mtakatifu kupitia ubatizo, miaka minne baada ya kuanza
safari yake ya wokovu.
Kush Tracey kupitia ukurasa wake wa Instagram,
alichapisha video akifanyiwa ubatizo kwenye dimbwi la maji ambapo alisema kwamba
imekuwa ni safari ya miaka 4 ambayo hawezi kuijutia hata kidogo.
Alifafanua kwamba miaka 4 iliyopita, alipokea ubatizo
wa roho mtakatifu lakini sasa ,amepokea ubatizo wa maji kusimika kabisa
uhusiano wake na Mungu.
“Imekuwa
miaka 4 ya kutembea na Bwana & Mwokozi wangu Yesu Kristo🥳 na tangu
nilipopokea Ubatizo wa Roho Mtakatifu (wakati Roho Mtakatifu anaingia katika
maisha ya waumini na kuwatia nguvu kwa ajili ya huduma ya Mungu) na leo
hatimaye nimebatizwa katika maji,”
Tracey alitangaza kwa furaha.
Alichukua
nafasi hiyo kuelezea uelewa wake kuhusu umuhimu wa ubatizo kwa Wakristo.
“Ubatizo maana yake halisi ni
kuzamishwa kabisa na ni ishara ya nje ya mabadiliko ya ndani ambapo mtu
hujitangaza hadharani kuwa ni wake na kujitambulisha na Yesu Kristo kwa kawaida
hufanyika baada ya mtu kuwa mwamini mpya ambaye amezaliwa mara ya pili.”
Hata hivyo,
kwa kutumia vifungu vya Biblia, Tracey alifafanua kwamba ubatizo katika maji si
njia ya pekee ya mtu kujenga uhusiano wake na Mungu kupitia kuamini katika
uwepo wa maisha baada ya kifo.
Alisema
kwamba wakristo hata baada ya ubatizo, wana jukumu la kutumikia wokovu wao kwa
woga mkuu mbele pa Mungu, akitoa kifungu hicho kwenye kitabu cha Wafilipi 2:12.
Mnamo mwaka
2021 wakati alifunguka kwa mara ya kwanza kuhusu uamuzi wake wa kutafuta maisha
mapya katika Ukristo, Tracey alifichua kwamba maisha yake yalikuwa yamechukua
mkondo mbaya usioweza kuelezeka.
Alipoulizwa kwa nini aliokolewa, Kush alisema;
"Nilikuwa nimegonga mwamba sana, watu wangeniona kwenye TV na
kwenye mitandao ya kijamii lakini nyuma ya hapo nilikuwa nikipambana na hisia
tofauti.”
“Nilihisi kuna maisha zaidi na kuwepo kwangu mbali na kuachilia muziki
na kujulikana. Nikifa leo watu wangesema nini kunihusu?”
“Nilihitaji kupata zaidi na kuishi katika kusudi na ningeweza tu kupata
hiyo katika Kristo. Kuwa Mkristo ni ngumu sana, unapaswa kuwa na nia na kila
mtu. Huwezi kutenda jinsi unavyotaka, kuwa Mkristo ni dhabihu kubwa ambayo ni
ngumu kufanya maishani mwangu."
Kuhusu kama alijisikia kukaribishwa na Wakristo wengine
katika tasnia ya burudani, Kush Tracey alishiriki;
“Kwangu mimi wokovu haukuwa wa watu kunikubali, watu wanafanya mambo kwa
sababu wana ajenda tofauti. Kuna watu wapo hapa kwa ajili ya biashara, wengine
ni waaminifu kwa Mungu. Ninaamini katika kufuata kile ambacho Mungu ameniitia
kufanya.”
“Mungu amekuwa akiniunganisha na mambo, Wakati kitu kinatoka kwa Mungu
huna haja ya kukipigania."