MPENZI wa Marioo, Paula Kajala amefichua kwamba
katika maisha yake anatamani sana Marioo amuoe rasmi katika harusi, huku
akiyapa masomo nafasi ya pili katika maisha yake.
Akizungumza kwenye mahojiano na Clouds Media, Paula
alisema kwamba angetaka sana kuolewa kwanza kisha masomo yaje baadae.
Alipoulizwa kuhusu elimu yake, Paula alifichua kwamba
japo aliachia masomo ya fasheni njiani, ana azma ya kuenda kumalizia masomo
yake pindi binti yao Amarah atakapokua.
“Nitaendelea
na masomo, nasubiri Amarah akue kwanza. Hiyo inawezekana. Mimi nataka niendelee
kusomea fasheni kwa sababu ndicho kitu ambacho nakipenda. Ninataka kujiendeleza
kwenye hilo,” Paula Kajala alisema.
“Hata
hivyo bado mipango ya ndoa naitaka sana. Nataka kuolewa kwanza masomo baadae,”
aliongeza.
Marioo alipoulizwa kuhusu hoja hiyo ya mpenzi wake,
alikiri kwamba ni suala la muda tu kwani sehemu kubwa wameshaifanya tayari
ikiwa ni pamoja na kuonana na kujuana na wakwe, katika shughuli ya kutambulisha
jinsia ya mtoto wao miezi michache kabla ya kuzaliwa kwake.
“Suala
na ndoa ni jambo jema, na sisi tumeshakuwa familia. Katika vitu vilivyotokea
hapa, ina maana suala la ndoa ni suala dogo sana. Ni suala tu la kuamua, na
sheria tuwe tushaifuata maana vitu vingi vya msingi tumeshavifanya kwa hiyo
imebakia tu sisi kusema kwamba jamani tarehe Fulani tunataka tuoane, tufunge
pingu za maisha,” Marioo alikariri kauli ya mpenziwe.
“Nitamuoa
kwa sababu mwanzo nampenda, pili amenizalia binti mzuri na naheshimu uamuzi
wake. Kwa hivyo, kama hitaji lake ni ndoa tu hilo ni suala dogo na limeisha,”
Marioo aliongeza.
Katika video ya mahojiano hayo, Paula alionekana
akiwa bila kujipodoa na alipoulizwa, alisema kwamba tangu awe mzazi, hapendi
kutumiwa vipodozi, akikiri kwamba hiyo ni baada ya kutambua kuwa yeye ni mrembo
bila kujipodoa.
“Situmii make-up kwa sababu mimi ni mzuri tu jinsi nilivyo. Sio kama sipaki make-up, lakini natumia tu mara moja moja. Na Marioo hapendi nipake make-up. Nikipata make-up huwa ananichamba,” Paula alisema huku Marioo akitilia mkazo kwa kusema, “Mimi namuona akikaa hivyo anakuwa sawa tu. Japo naunga mkono huo urembo wa kujiongeza lakini akikaa hivi jinsi alivyo anakaa mzuri zaidi.”