MTANGAZAJI na msanii wa
nyimbo za injili za Kikamba, Mercy Mawia aliyefariki mwishoni mwa mwezi Julai
ameachia wimbo wake mpya.
Mawia, ambaye alikuwa
mtangazaji katika kituo cha redio ya Mbaitu FM inayotangaza kwa lugha ya
Kikamba alifariki Julai, na miezi minne baadae, mumewe James Mwangi ameachia
wimbo wake wa mwisho.
Mwangi, kupitia ukurasa
wake wa Facebook, alifichua kwamba wimbo huo ulikuwa wa mwisho uliorekodiwa na
Mercy kabla ya kifo chake.
Mwangi ameachia iwmbo
huo siku ambayo ilifaa kuwa siku ya kuzaliwa ya mpenzi wake, Mercy Mawia ambayo
ni Novemba 29.
“Katika maisha yake,
mwanamume atamlilia mwanamke mmoja tu. Baada ya hapo, hawezi kamwe kuingia
katika upendo tena,” Mwangi alisema huku akifichua
kuachia wimbo huo.
Mnamo Julai 23, Kituo
hicho cha redio kilithibitisha kifo cha mtangazaji huyo na kuongeza kuwa aliaga
dunia alipokuwa akifanyiwa upasuaji. Mumewe alikuwa kando yake wakati kwa
bahati mbaya aliaga dunia.
"Ni kwa masikitiko makubwa tunatangaza kifo cha ghafla cha mtangazaji wetu wa kipindi cha Drive Show Mercy Mawai. Mercy almaarufu Kamuwetangi, amefariki asubuhi ya leo alipokuwa akipatiwa matibabu," kituo hicho kilitangaza