MFANYIBIASHARA Shakib Cham Lutaaya ametoa onyo kali kwa
baadhi ya wanablogu wanaoeneza taarifa alizozitaja kama uvumi kwamba anachepuka
katika ndoa yake.
Kupitia kwa aya ndefu alizochapisha kwenye ukurasa
wake wa Instagram kupitia insta-story, Shakib alisema kwamba amekuwa akifumbia
macho tetesi hizo kwa muda lakini sasa anaona kimya chake kinachukuliwa kama
unyonge.
Shakib alisema kwamba hajui mtu aliyebuni na kuibuka
na uvumi kwamba ana mpenzi mwingine nje ya ndoa yake na Zari, na kukanusha
taarifa hizo akizitaja kuwa za kupotosha.
"Wapendwa wa mitandao ya kijamii na mashabiki, ningependa
kushughulikia suala linalonihusu kuhusu uvumi wa hivi majuzi wa magazeti ya
udaku kwamba nina uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa yangu. Imefika akilini
mwangu kuwa kumekuwa na hadithi za uwongo zinazosambaa zikionyesha kuwa
ninamsaliti mke wangu,” Shakib alisema.
Akizungumzia kuhusu baadhi ya wanawake anaoonekana nao na
ambao sekeseke zilikuwa zinadai kuwa ni wapenzi wake, Shakib alisema kwamba wao
ni wateja wake katika duka lake la nguo.
"Nataka kuweka mambo wazi, baadhi ya wanawake ni wateja wa thamani
na wafuasi wa ukusanyaji wa King Cham. Hawajihusishi nami kimahaba, wala sina
nia yoyote ya kujihusisha na mahusiano ya faragha nao au wanawake wengine
wowote kwa jambo hilo. Kama mwanamume aliyeoa, mapenzi yangu na kujitolea viko
kwa mke wangu,” alisisitiza.
Zaidi ya hayo, Shakib aliwasihi mashabiki na wafuasi wake
kupuuza madai hayo akiyaita uvumi na propaganda zisizo na msingi ambazo
zingedhuru ndoa yake.
"Ninaomba kila mtu tafadhali ajiepushe kueneza uvumi na propaganda
hizi zisizo na msingi, kwani sio tu sio za kweli lakini pia zinadhuru kwa ndoa
yangu, sifa ya kibinafsi na kitaaluma. Hebu sote tuonyeshe kuelewana na
kuheshimiana.”
Zari na Shakib wameoana kwa mwaka mmoja, baada ya kufunga
ndoa ya Kiislamu – nikkah – iliyofanyika faraghani mwaka jana.
Baadae mwezi Oktoba, waliweka mambo wazi kwa kuandaa sherehe
kubwa ya harusi nchini Afrika kusini.
Harusi hiyo ya kifahari ilihudhuriwa na watu mashuhuri na
baadhi ya wasanii wa Young Famous na Afrika.
Hata hivyo, unaambiwa sio vyote ving’aavyo ni dhahabu. Ndoa ya
wawili hao imekumbwa na misukosuko si haba katika kipindi hicho, suala luu la
ugomvi likiwa ni ukaribu wa Zari na babydaddy wake, Diamond Platnumz.
Miezi michache iliyopita, Shakib na Zari walitupiana maneno
ya kejeli kwenye mitandao ya kijamii baada ya Zari kumualika Diamond kuhudhuria
siku ya kuzaliwa ya binti yao, Tiffah.
Video kutoka kwa tafrija hiyo zilimuudhi Shakib ambaye
alimsuta Zari kwa kuendekeza hisia kwa Diamond licha ya kuwa tayari walisha
achana muda mrefu – 2018.
Zari alikanusha madai hayo akisema kuwa ujio wa Diamond
katika tafrija ya siku ya kuzaliwa binti yao ilikuwa jambo la kushtukiza kwani
hata yeye mwenyewe hakuwa na taarifa.
Zari alimfokea Shakib kwamba alikuwa ni mtu mwenye mashaka
tele katika uhusiano wao, akimtaka kukomaa na kujua kwamba uhusiano wake na
Diamond si kitu chochote zaidi ya kushirikiana kuwalea watoto tu.