Msanii wa Amapiano ya Kiswahili kutoka Tanzania,
Chino Kidd ameahidi kumpa shavu rapa wa humu nchini Stevo Simple Boy.
Akizungumza katika mahojiano kwenye runinga ya TV47, Chino
Kidd alisema kwamba angependa kumsaidia Stevo Simple kwa kutimiza moja ya ndoto
zake ambayo ni kukutana na Diamond kwa ajili ya kolabo.
Chino Kidd alifafanua kwamba yeye yuko tayari kwa
asilimia 100 kushirikiana na Stevo Simple Boy kwenye kolabo lakini pia
kumpeleka moja kwa moja hadi kwa Diamond Platnumz.
Aliyasema hayo baada ya Dr Ofweneke kumuuliza kama
anaweza kumsaidia Stevo Simple Boy, aliyempigia debe kama kijana mwenye talanta
ambaye amejituma sana kimuziki.
“Mimi
ninaweza fanya muziki na Stevo Simple Boy 100% na nitambeba pia nitaenda naye
Tanzania na hata kumkutanisha na Diamond.
Lakini pia nitafanya naye interview kule kwa sababu watu wanamfahamu
kule, mimi mwenyewe nilimjua na nikamfollow,”
Chino Kidd alisema.
Hata hivyo, msanii huyo alisema kumkutanisha Stevo na
Kajala ni nje ya uwezo wake kwa kile alichokitaja kuwa aliwahi kumsema vibaya
Harmonize – ambaye bado anaonekana kuvutiwa na ex wake, Frida Kajala katika
siku za hivi karibuni.
Iwapo Chino atafanikisha kumkutanisha Stevo na
Diamond basi itakuwa ni ndogo iliyofaulu kwa msanii huyo ambaye miezi michache
iliyopita alimtania Diamond kwamba angemtoza hela ndefu ili kufanikisha kolabo.
"Diamond, ulinitumia meseji
kwenye Instagram ukisema unataka collabo, lakini usipokohoa Sh20 milioni,
hakuna dili,” Aliyejitangaza Mfalme wa Afrika, Stevo Simple Boy alisema.
Wiki mbili baadae, msanii huyo alilazimika
kutetea uamuzi wake wa kudai milioni 20 ili kupata kolabo na Diamond.
Kulingana na Simple Boy, Wakenya wamechangia pakubwa
mafanikio ya Diamond kimuziki.
“Ni kweli nilisema hivyo kwa sababu ukitutazama sisi
Wakenya tumemuunga mkono Diamond mpaka amefikia, kwanini asirudishe mkono wake
na kufanya kolabo na msanii wa Kenya? Steve alisema.
Msanii huyo pia alienda mbali zaidi na kufichua kuwa
kauli hiyo iliwatia kiwewe Watanzania kiasi kwamba vyombo vingi vya habari
kutoka nchini humo vilimtafuta kwa njia ya simu kumtaka aeleze zaidi.
“Vyombo vya habari vya Tanzania vilinipigia simu,
vikisema Steve umefanya jambo la maana kwa sababu tunaona kazi yako Kenya, wakasema
pia Diamond ana haki ya kutoa Sh20m hivyo nimpe ushirikiano,” alieleza.
Kwa mara kadhaa, msanii huyo wa Kenya amekuwa
akijinadi kama Diamond wa Kenya.
“Najua Wakenya na watu wengine walikuwa wanasema eti mimi ni Diamond wa
Kenya. Kwa hiyo mimi nilikuwa nasema hizo zikitulia naachilia ngoma, unaona.”