MTANGAZAJI wa Radio Jambo, Joe Gidi amekanusha madai
yanayoenezwa mitandaoni kwamba alipoteza wafuasi wengi kwenye jukwaa la YouTube
baada ya kutumbuiza katika sherehe za Jamhuri, Desermba 12.
Akizungumzia uvumi huo kwa mara ya kwanza kupitia
ukurasa wake wa Facebook, Gidi alisema kwamba taarifa hizo hazima mashiko na
kuzitaja kama porojo zinazoendeshwa na wanablogu kutafuta kiki tu mtandaoni.
Taarifa ambazo zimekuwa zikisambaa baada ya Gidi
kutumbuiza katika sherehe za Jamhuri ni kwamba alipoteza wafuasi zaidi ya 10k
YouTube saa chache baada ya sherehe hizo kukamilika.
Gidi alikanusa uvumi huo akisema kwamba hata chaneli
yake ya YouTubew haijawahi fikisha wafuasi 10, achia mbali kuwapoteza wafuasi
hao.
Alisema kwamba yeye hajawahi tyumia kurasa zake
kwenye mitandao ya kijamii kutengeneza pesa, akisisitiza kwamba huitumia tu
kujivinjari na pia akaweka wazi kuwa yeye mara nyingi hutumia mtandao wa
Facebook.
“Nimeona
baadhi ya TikTokers na wanablogu wakitumia hadithi hii bandia kwenye maoni yao.
Situmiki kwenye YouTube na sijawahi kuwa na wafuasi 10k. Sipokei mapato ya
mitandao ya kijamii, ninaitumia tu kwa maoni ya kijamii. Ninafanya kazi kwenye
facebook pekee. Jihadhari na kupuuza habari ghushi zinazoundwa na watu
wanaotafuta kupenda na ubofye chambo mtandaoni,”
alisema.
Sherehe za Jamhuri zilifanyika jijini Nairobi katika
uwanja wa Uhuru Gardens ambapo Gidi alikuwa miongoni mwa wasanii wakongwe
waliotumbuiza kuadhimisha miaka 61 ya Kenya kujitawala.
Pindi tu ilipobainika kwamba mtangazaji huyo maarufu
wa kipindi cha Patanisho alikuwa kwenye orodha ya watumbuizaji wakongwe,
Wakenya haswa kwenye mtandao wa X walianzisha kampeni za kumshambulia na
wengine hata kumtumia jumbe zisizofurahisha kwenye simu yake.
Hata hivyo, Gidi alionekana kutoyumbishwa na
mashambulizi hayo ambayo siku ya Jamhuri alitoa moja la tumbuizo la kuvutia
akiwa na mwenzake, MajiMaji ambaye walikuwa wanaimba naye.
Kabla ya kujizolea umaarufu kama mtangazaji kwenye
Radio Jambo, Gidi alikuwa msanii wa kibabe mapema miaka ya 2000s akiwa na
MajiMaji ambapo miongoni mwa vibao vyao vingi, ‘Unbwogable’kinasalia kuwa kibao
kilichowatambulisha zaidi kwa Wakenya wa matabaka mbalimbali.