MSANII wa kizazi kipya, Maandy amekuwa wa hivi punde kutoa tamko kuhusu vita vya maneno kati ya wasanii wa Gengetone na wale wa Arbantone.
Mzozo huo uliibuka pindi tu kikundi cha Gengetone,
Ethic Entertainment walipotangaza wiki jana kwamba wangerudi pamoja kufanya
muziki, miezi kadhaa baada ya kutengana.
Ujio wao ulivutia vita vya maneno kutoka kwa wenzao
wa Arbantone, baadhi wakionekana kukejeli ujio huo huku wengine wakiwaunga
mkono kwa kufanya uamuzi wa kurudi pamoja.
Hata hivyo, mzozo huo umeonekana kumchukiza Maandy
ambaye amewataka wasanii kutoka pande hizo mbili kuheshimiana na kushirikiana
badala ya kuanzisha vita vya kibabe.
Maandy anahisi kwamba muziki wowote uwe Gengetone au
Arbantone ni mzuri tu ukifanywa vizuri haijalishi na nani, na kuwataka wasanii
hao kushirikiana badala ya kusutana.
“Tunaweza
komesha kabisa aya yote ya sijui ni nani amerudi, ni nani ameenda, ni nani
amefanya au ameimba…tunaweza ishi vizuri pamoja sisi wote. Kama hauhisi
kutishiwa, haufai kuingilia hayo mambo. Muziki ni muziki tu bora ni noma,”
Maandy alishauri kupitia Instagram.
Kauli yake inajiri siku mbili tu baada ya kushuhudiwa
kutupiana maneno baina ya DJ wa Gengetone VDJ Jones na msanii wa arbantone, YBW
Smith kuhusu ni muziki upi bora kati ya gengetone na arbantone.
Baada ya Ethic kurudi na kuachia wimbo huo, hizi hapa
ni baadhi ya kuali kutoka kwa wasanii wa Arbantone;
“Napata DMs kwamba Gengetone imerudi, labda hawa
wagenge wastone. Shindano la 1v1 likuje basi,” YBW Smith aliandika.
“Sikatai wamerudi, lakini watawezana na mimi kweli,”
Tipsygee aliuliza.
“Heshima kwa wasanii wa gengetone lakini mistari kwa
mistari hakuna anayeniweza,” alisema Sosa the prodigy.
‘Kusema ukweli mimi ninahisi kama gengetone
itafufuka, litakuwa ni jambo zuri zaidi. Najaribu kutafakari tamasha la
gengetone dhidi ya arbantone. Na kwa kuongezea, arbantone tunahitaji huu ujio
wa gengetone ili kuimarika zaidi,” Sean MMG alisema.