MCHEKESHAJI Kendrick Mulamwah kwa mara ya kwanza amevunja kimya kuhusu madai yanayoendelea mtandaoni kuusu gari lake kupigwa mnada lakini pia kuwa na deni kubwa la benki.
Madai hayo yamekuwa yakienezwa katika mitandao ya
kijamii tangu mwaka uanze na chanzo chake hakijulikani, huku kila mtu
akionekana kuwa na maoni yake kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa Facebook,
Mulamwah alizungumzia suala hilo kwa mara ya kwanza baada ya kugundua kwamba
lilikuwa suala la mjadala pevu katika ukurasa mmoja kwenye TikTok.
Mtu mmoja kwenye TikTok hata alidai kwamba Mulamwah
anadaiwa na benki zaidi ya shilingi milioni 35 ambazo mtu huyo alidai kuwa
alizitumia kujenga nyumba na kununua gari.
Hata hivyo, Mulamwah aliyeonekana kushangazwa na
suala hilo alipigwa na butwaa kuona mtu huyo akiorodhesha takwimu hizo
zilizomshangaza pia.
“Eeish,
mmesema milioni 35?” Mulamwah aliuliza kwa mshangao.
Mchekeshaji huyo kutoka Magharibi mwa Kenya
alitangaza kununua gari jeusi aina ya Mercedes Benz mwaka jana mwezi Machi.
“MUNGU
ALIFANYA 💪🙏 mmiliki wa gari la fahari 💯 mercedes BENZ E250. Kila mara tembea
polepole lakini sogea ipasavyo, inanipasa kumshukuru Mungu kwa baraka zote
maishani. Wacha tuanzie maisha hapa. Asante kwa familia, mashabiki na marafiki
kwa usaidizi wenu na maombi kila wakati,” Mulamwah
alisema.
Baba huyo wa mtoto mmoja alisema kwamba
sasa angalau mkewe Ruth K atakuwa anamwahisha mtoto kliniki kwa muda wakiwa
ndani ya gari.
“Kijana wa kitale sasa ni former pedestrian.
Kalamwah na mama Kalamaz sasa watakuwa wanafika kliniki kimtindo. @atruthk
asante kwa support daima mamake,” alisema.
Hata hivyo, huenda madai hayo yakawa si ya kweli,
kwani mwishoni mwa mwaka, mchekeshaji huyo alionyesha zaidi ya milioni moja
alizokuwa amewekeza ndani ya kibubu kwa muda wa miezi 12.
Akiwaasa wenzake kuwa na mpango wa kuwekeza, Mulamwah
alifichua kwamba alikuwa anawekeza kiasi cha shilingi elfu 3 kila siku kwa
mwaka mzima.