BOSI WA LEBO ya Konde Music Worldwide, Harmonize amefichua kwamba ombi lake mwaka huu ni kuongeza mtoto mwingine.
Msanii huyo ambaye ni baba kwa binti mmoja kwa jina
Zuhu, alifichua kwamba angependa kuongeza mtoto mwingine wa kike mwaka huu ili
kuwa ndugu mdogo kwa binti wa kwanza.
Alisema kwamba iwapo atapata mtoto huyo, atampa jina ‘Furaha’
kuashiria furaha aliyo nayo kuwa baba kwa mara nyingine tena.
Harmonize amekuwa akijishebedua na watoto wawili wa
kike, Zuhu na binti wa mpenzi wake wa zamani wa Poshy Queen kwa jina Nova
ambaye anampenda licha ya kuachana na mamake miezi michache iliyopita.
Harmonize alifunguka kwamba mabinti zake Zuhu na Nova
sasa wanafaa kujiweka tayari kwa binti yao mwingine ajaye, Furaha.
“Ombi
langu Mungu baba, natamani sana nipate mtoto wa kike 2025. Mitamuita Furaha.
Zureha na Nova tunakungoja wewe Furaha,” Harmonize
aliandika.
Hata hivyo, Harmonize hakuweza kubainisha ni jinsi
gani atapata mtoto huyo bila ya kuwa na mpenzi, lakini kama wanavyosema, penye
nia pana njia.
Msanii huyo hajakuwa na bahati kimapenzi kwani
amekuwa akiingia na kutoka katika mapenzi licha ya kuonekana kujitutumua.
Alianza mapenzi na Wolper ambaye ameachana juzi na
mume wake wa ndoa, Rich Mitindo kabla ya kumpenda raia wa Italia Sarah
Mitchelotti na baadae Kajala Masanja mara mbili, lakini hakuna penzi
lililodumu.
Mwaka jana, alitangaza kuingia katika huba na mrembo
Poshy Queen ambaye licha ya kuongozana naye hadi kanisani na kufananisha nguo,
penzi hilo halikuweza kuona mwishoni mwa mwaka kwani lilisambaratika vipande
vipande.
Licha ya kutendwa kimapenzi mara kadhaa, Harmonize
yuko mbioni tena kujaribu karata tata katika uwanja wa mapenzi, safari hii
akiwa na tumaini la kutoka na mtoto wa kike, na si mikono mitupu.