MFANYIBIASHARA Zari Hassan amejitokeza na kufoka vikali dhidi ya watumizi wa mitandao ya kijamii wanaokejeli na kukosoa Kiingereza cha mumewe, Shakib Cham Lutaaya.
Zari na Shakib ni miongoni mwa mastaa waliojumuishwa
kwenye msimu wa tatu wa kipindi cha uhalisia cha Young, Famous & African
kwenye jukwaa la utiririshaji la Netflix.
Kionjo cha kipindi hicho ambacho kitapeperushwa
Januari 17 kilichapishwa mitandaoni wiki iliyopita na watumizi wa mitandao ya
kijamii haswa kutoka Afrika Mashariki walikuwa wa haraka kukejeli Kiingereza
cha Mganda huyo.
Hata hivyo, Zari ameamua kuvunja kimya na kunyoosha
mtutu wa bunduki ya maneno kwa wakosoaji hao akisema kwamba wataishia tu
kukosoa Kiingereza kibaya cha mumewe mitandaoni lakini yeye tayari
ameshafanikiwa kuingia kwenye jukwaa hilo kubw zaidi la kutiririsha video.
“Eti
ooh, hatutangoja kuona na kusikia Kiingereza cha SHAKIB… achene sasa tuzungumze
kuhusu hicho Kiingereza. Acha tuzungumze! Acha niwaambie kitu, huu umekuwa ni
msimu wa ushindi kwa mume wangu. Kwa kunioa, mume wangu aliangukia na huu
umekuwa msimu wake wa kuvuna pakubwa,” Zari
alisisitiza.
“Mume
wangu ataonekana kwenye Netflix, lakini wewe hapo na Kiingereza chako kizuri,
chenye lafudhi ya kuvutia na ujuzi wa kipekee, jiangalie! Mume wangu anaenda kuonekana kwenye
jukwaa kubwa zaidi duniani la video – Netflix, na wewe utashinda hapo. Hata hujihurumii!”
Zari aliwapalia makaa wakosoaji.
Mama huyo wa watoto watano alizidi kumvisha koja la
maua mume wake akisema kwamba hata alijizolea umaarufu maradufu kumliko baada
ya kuonekana naye kwenye Netflix.
Alimshauri mfanyibiashara huyo wa nguo kutoka Uganda
kutokwazwa na maneno ya watu mitandaoni, na kumtaka siku zote kuzikita mbona zake
kwenye zawadi kuu ya kutafuta hela.
“Na
kupitia kuonekana kwenye Netflix, si siri kwamba dili kubwa zitabisha sasa. Nani
anayejua, pengine mume wangu hata atanipita na pengine kufika Hollywood. Mpenzi
wangu usiyumbishwe, na kwenu nyinyi mabibi na mabwana, huu ni msimu wa ushindi
kwa Shakib. Nina furaha kubwa kwake.”
“Sijawahi
mpenda mtu mwingine kama ambavyo nimempenda Shakib na kuona nyota yake iking’aa
hivi,” Zari aliongeza.
Hii ni mara ya kwanza kwa Shakib kutokea kwenye
kipindi hicho kwani msimu wa kwanza na wa pili miaka miwili iliyopita, Zari
aliigiza na aliyekuwa mumewe, Diamond Platnumz.