
WIKI chache baada ya Netfix kuachia msimu wa tatu wa filamu ya uhalisia, Young Famous & African, Wakenya mbalimbali wamejitokeza na kuonyesha kutoridhishwa kwao jinsi hakuna Mkenya hata mmoja amefanikiwa kujumuishwa tangu mswimu wa kwanza mwaka 2022.
Malalamiko haya yametoka si tu kwa Wakenya wa kawaida pekee
lakini pia maceleb mbali mbali ambao wamesimama kidete kuwapigia debe maceleb
wenzao ambao wanaona wana vigezo sawa na wale waliojumuishwa kwenye kipindi
hicho cha Netflix.
Siku chache zilizopita, mmoja wa mastaa kwenye kipindi
hicho, mfanyibiashara Zari Hassan alikuwa humu nchini ambapo alikuwa mtu wa
kwanza kutoa maoni kuhusu ni Mkenya yupi anayestahili kwenye Young, Famous
& African.
Zari alimpigia upato mwanasosholaiti Vera Sidika kujumuishwa
kwenye msimu ujao, akisema kuwa anastahili pamoja na mvuto wake kwenye mitandao
ya kijamii na pia umbile lake la kipekee.
"Vera
angeonekana mzuri kwenye onyesho letu. Ninahisi kama yeye ni mrembo, analeta
nyash yote, na ninahisi kama anaweza kurusha miguno. Vera, anafanana na
sisi," Zari alisema.
Ungamo la Zari
kuhusu Vera lilifungulia mirija ya maoni kutoka kwa maceleb wengine wa Kenya
ambapo, Chiki Kuruka, mke na meneja wa msanii Bien naye alitoa maoni
akimpendekeza msanii Chimano Willis kama karata bora ya kuwakilisha Kenya
kwenye YFA.
Kwa mujibu wa
Kuruka, Chimano ana kila kigezo cha kugeuza vichwa mara mbili mbili kwenye
kipindi hicho cha uhalisia kwa fasheni yake ya kipekee.
“Mpendwa @youngfamousandafrican Kipindi chako ni
CHA AJABU! Kitu pekee ambacho kingeifanya kuwa bora zaidi, itakuwa uwepo wa
@willis.chimano Tafadhali zingatia! Kutoka kwa shabiki mwenye shauku,” Chiki aliandika kwenye chapisho lake.
Kama hiyo haitoshi, msanii wa kundi la
Wakadinali, Scar Mkadinali naye hakuachwa nyuma kwa maoni yake kuhusu Mkenya
anayehisi anastahili kupewa nafasi kujumuika na mastaa wengine wa Kiafrika
kwenye YFA.
Scar Mkadinali alimpendekeza rapa
mwenzake, Skillo, akisema ndiye chaguo bora atakayeonyesha ubora wa kiuhalisia
wa tamaduni za Wakenya.
“Wapendwa Young Famous & African,
kipindi chenu ni cha ajabu! Kitu pekee ambacho kitafanya kipindi kuwa bora zaidi
ni kumuongeza Skillo. Kutoka kwa Rong Rende tunawapa Skillo,” Scar alipendekeza.
Skillo Kenyan ni
rapa wa Kenya, anayejulikana kwa muziki wake wa hip-hop, mara nyingi akitumia
"@loskiskillo" kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii kama Instagram;
anachukuliwa kuwa msanii anayechipukia katika tasnia ya muziki ya Kenya, haswa
katika jamii ya Wajaluo.