MCHEKESHAJI aliyegeukia uanaharakati, Eric Omndi amevunja kimya chake siku moja tu baada ya watu wanaoaminika kuwa kutoka katika uongozi wa serikali ya kaunti ya Turkana kubomoa darasa alilojenga miezi michache iliyopita.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Omondi alionyesha
kusikitishwa kwake na hatua hiyo iliyoonekana kutumbukiza kwenye maji juhudi
zake kupitia kwa wakfu wa Sisi Kwa Sisi.
Alisema kwamba inashangaza kuona serikali ilirudisha nyuma
hatua za misaada ya kibinadamu kutoka kwa wahisani wema wakati serikali hiyo
yenyewe imeshindwa kwa muda mrefu kukidhi mahitaji muhimu kwa watu wake hadi
kuvutia jicho la huruma kutoka watu wa mbali.
“Inasikitisha sana
Walibomoa Darasa tulilojenga kwa ajili ya watoto lakini MBAYA zaidi watoto
walinyanganywa Uniform na Viatu...Hawa watu hata ni binadamu?” Eric Omondi alihoji.
Tukio hilo limezua hasira na masikitiko miongoni mwa
wanajamii, ambao walikuwa na matumaini kwamba muundo huo ungetumika kama nyenzo
ya kielimu inayohitajika sana kwa watoto wa eneo hilo.
Darasa hilo, ambalo lilijengwa na Omondi kama sehemu ya
juhudi zake za hisani kusaidia elimu katika maeneo yaliyotengwa,
lilisherehekewa na wakaazi kama mwanga wa matumaini.
Zaidi ya hayo, watoto wa Turkana wanakabiliwa na changamoto
kubwa katika kupata elimu, hasa katika maeneo ya mbali, na darasa lilionekana
kuwa suluhu yenye matokeo kwa uhaba wa nafasi za kujifunzia.
Shule hiyo ilipewa jina la mwalimu huyo ambaye amekuwa
akijitolea kuwafundisha wanafunzi hao bure.
“Tuliita shule hiyo Shule ya Msingi ya Mwalimu Kamaret baada
ya mwalimu wa ajabu aliyejitolea kuwafundisha watoto hawa. Tulifanikiwa kumpa
posho ya kumkimu kwa angalau miezi miwili,
"Bado mengi yanahitajika kufanywa kwa sababu zaidi ya
nusu ya watoto bado hawana sare, na darasani halijakamilika kwa asilimia 100.
Mwishoni mwa mwaka huu, tutakuwa na shule kamili hapa na vifaa vya bweni. Mungu
akubariki,” alisema Omondi baada ya misheni.