RUNINGA ya shirika la Habari la taifa, KBC imethibitisha kwamba ukurasa wao wa mtandao wa uko mikononi mwa wadukuzi, saa chache baada ya watumizi wa X kutilia shaka machapisho yao.
Katika taarifa kwenye ukurasa wao wa
Facebook, KBC walisema kwamba ukurasa wao wa X umedukuliwa na kufichua kwamba
juhudi za kuurudisha mikononi mwao zinaendelea.
KBC iliomba samahani kwa mashabiki
wao kutokana na machapisho ambayo yaliyochapishwa kwenye ukurasa huo, wakitoa
tahadhari kuu kwamba hayatoki kwao.
“Tahadhari: ukurasa wa KBC
Channel 1 kweny X umedukuliwa na tuko katika mchakato wa kuurudisha mikononi
mwetu. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote
na tunatoa ushauri wa watu kuwa makini wanapotangamana na ukurasa huo haswa
machapisho ya hivi majuzi,”
walisema huku wakiwataka mashabiki wao kufuatilia Habari zao kupitia ukurasa wa
Facebook.
Hii si mara ya kwanza kwa wadukuzi
kuteka kurasa za mashirika na idhaa mbalimbali humu nchini.
Mwaka jana, klabu ya soka ya KCB inayoshiriki
ligi kuu ya humu nchini, FKF-PL walitangaza kudukuliwa kwa ukurasa wao wa
Facebook.
Tangazo hilo lilijiri miezi kadhaa
baada ya klabu nyingin, Shabana FC pia kutangaza kudukuliwa kwa ukurasa wao wa
Facebook.
Chuo kikuu cha Kabarak pia
hakikusazwa katika udukuzi huo ambapo walipoteza ukurasa wao wa Facebook kwa
siku kadhaa kabla ya kufanikiwa kuurudisha mikononi mwao.