SHAKIB Cham Lutaaya, mfanyibiashara wa Uganda ambaye pia ni mume wa mwanasosholaiti na mjasiriamali Zari Hassan kwa mara ya kwanza amejibu swali la wengi kuhusu alichokifanya kwenye Netflix.
Shakib, ambaye kwa mara ya kwanza
katika Maisha yake alitimiza ndoto ya kuonekana kwenye filamu ya Netflix –
Young Famous & African, ameelezea kwamba alichokifanya wakati wa
kujitambulisha hakikutokea kwa bahati mbaya bali ni jambo ambalo alikuwa akifikiria
kwa muda na alifanya hivyo kwa kusudi moja.
Mfanyibiashara huyo ambaye pia ni
bondia alifanya mahojiano ya kipekee na kituo kimoja nchini Uganda alipoeleza
sababu ya yeye kujitambulisha kwa Kiganda wakati kila mtu alikuwa anatumia
lugha ya Kiingereza.
Kwa mujibu wa Shakib, kujitambulisha
kwa Kiganda hakukumshusha hadhi kwa njia yoyote kama ambavyo baadhi walihisi
kwani alijionea Fahari kuipeleka lugha yake ya nyumbani kwa mamilioni ya watu
wanaofuatilia kipindi hicho kote duniani.
Alisema kwamba tangu utotoni, alikuwa
akifuatilia filamu na alihisi wakati ajapopata nafasi, ataifanya kwa lugha ya
nyumbani kama njia ya kuonyesha fadhila kwa lugha iliyomkuza.
“Nimekua tangu utotoni
nikifuatilia filamu za Netflix na nilikuwa nikitamani siku nitaona filamu za
Uganda kwenye jukwaa hilo. Hivyo wakati nilipata nafasi ya kuwa kwenye filamu
ya Netflix ya Young, Famous & African, nilitaka kupeperusha bendera ya Uganda
kwa kutumia lugha ya Luganda,”
Shakib alieleza.
Katika filamu hiyo ambayo iliigizwa
na matajiri wa fani ya burudani kutoka mataifa kadhaa Afrika, Shakib
alijitambulisha kwa lugha ya nyumbani na kuzua maoni kinzani haswa kutoka kwa
watu ambao hawana uelewa na lugha hiyo.
Suala hilo bila shaka linadhaniwa
kuwa moja ya sababu iliyomfanya mrembo kutoka Nigeria, Anne Macaulay, ambaye
hivi majuzi ametalikiwa na mumewe 2Face Idibia kumkejeli Mumewe Zari machoni pa
Zari mwenyewe.
Zari pia aliwafunga midomo baadhi ya
watu waliofurika kwenye mitandao ya kijamii wakikejeli Kiingereza cha Shakib
kilicho na lahaja nzito ya Kiganda.
Kwa mujibu wa Zari, huu umekuwa
wakati wa mavuno kwa mumewe na pengine wengi wanaokejeli matamshi yake hawana
chochote Zaidi ya simu na ufikiaji wa intaneti.