
MWANAMKE mmoja mwenye umri wa miaka 28 ameripotiwa kuwa na tatizo la figo zisizofanya kazi baada ya kudaiwa kula vyakula vyenye virutubishi vya Vitamini C kupita kiasi akitaka ngozi yake iwe laini.
Kisa hicho cha kutisha kilichapishwa na daktari
@drbelswellness kwenye X, ambaye alionya kuhusu kuongezeka kwa idadi ya masuala
yanayohusiana na figo miongoni mwa vijana kutokana na matumizi mabaya ya
virutubishi.
Kulingana na daktari huyo, mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka
28 hakuwa na historia ya kuvuta sigara, shinikizo la damu, au kisukari, lakini utendaji
kazi wa figo yake ulizorota haraka.
Uchunguzi wa kimatibabu baadaye ulionyesha kwamba alikuwa na
ugonjwa wa kidney stones, ambao ulisababisha maambukizo makali na
hidronephrosis.
Licha ya kupata matibabu, hali yake ilizidi kuwa mbaya na
hatimaye kuhitaji kupandikizwa figo.
Dadake alikubali kutoa figo yake moja ili kuokoa maisha
yake. Hata hivyo, madaktari walipochanganua figo zilizoondolewa, waligundua
kiasi cha kutisha cha oxalate kilichowekwa ndani yake—athari iliyohusishwa na
ulaji mwingi wa vitamini C.
Daktari huyo alisimulia;
"Tulikuwa na mwanamke mdogo mwenye umri wa miaka 28 ambaye alikuwa
akikabiliwa na kushindwa kwa figo. Hakuvuta sigara, wala hakuwa na shinikizo la
damu au kisukari. Kwa hivyo, ni nini kilisababisha mwanadada huyu kushindwa
kufanya kazi kwa figo? Alikuwa na baadhi ya mawe kwenye figo ambayo
yalisababisha pyelonephritis na hidronephrosis.”
"Tulianza matibabu, lakini iliendelea kuzorota haraka, kwa
mshangao wetu. Muda si muda alifikia hatua ya kuhitaji kupandikizwa figo.
Maisha ya msichana huyu yalikuwa yakienda polepole. Walitafuta wafadhili, na
dada yake alikuwa sawia. Kwa ridhaa, tulipanga upesi ili upandikizaji ufanyike
na tukatarajia bora zaidi.”
"Kupandikizwa kwa figo ya dada yake kulifanikiwa, na uchambuzi wa
figo ulipofanywa, ikawa kwamba kulikuwa na oxalates nyingi zilizowekwa kila
mahali kwenye figo zote mbili.”
"Aliporudi, tulijaribu kutafuta kilichosababisha hali hii, ili
kuzuia kutokea tena. Lakini maswali yetu yote hayakuzaa matunda, hadi
tulipouliza swali lililoonekana kutokuwa na madhara: Je, ulikuwa ukitumia
virutubisho vya Vitamini C mara kwa mara? Iligundulika ni kweli. Alikuwa
akichukua kiasi gani? Aliichukua kama kidonge, ilikuwa imechanganywa na unga wa
Glutathione ambayo alikunywa, na pia alichukua infusions mara kwa mara - yote
ili kuwa na ngozi inayong'aa.
“Hata aliendelea kuinywa tulipokuwa tukipambana kuokoa figo zake. Hii
ndiyo sababu iliendelea haraka. Dada yake aliachwa na figo moja kwa sababu ya
hii, lakini inaweza kuwa mbaya zaidi. Alikaribia kupoteza maisha. Tunaona visa
kama hivyo vya wale ambao hawakufanikiwa.”
"Sasa ulimwengu unashangaa kuhusu utunzaji wa ngozi na
kuwekeza sana katika virutubisho. Vitamini C inaweza kukufanya ung'ae, lakini
kuchukua zaidi ya miligramu 2,000 kwa siku kunaweza kuharibu figo zako! Tunaona
ongezeko la visa vya matatizo ya figo miongoni mwa vijana, na hii ni sababu
mojawapo.
“Dada yake angejisikiaje kujua ana figo moja tu kwa sababu ya kosa linaloweza kuepukika? Sio kosa la mtu kwa sababu hakupewa taarifa! Wacha tusaidie kueneza ufahamu: Virutubisho vinaweza kuua visipotumiwa kwa njia ifaayo."