
MKEWE Sergio Ramos, Pilar Rubio, ameripotiwa kuamua kutohamia Mexico kufuatia mumewe kuhamia klabu ya Monterrey siku ya Ijumaa.
Gwiji huyo wa soka wa Uhispania alitia saini mkataba wa mwaka
mmoja na timu yake mpya baada ya kukaa bila klabu kwa miezi sita.
Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 38 alionekana mara ya
mwisho uwanjani Mei 2024, akiichezea Sevilla katika mechi ya kichapo cha mabao
2-1 dhidi ya Barcelona kwenye LaLiga.
Kwa upande wake mpya, Mhispania huyo atavaa nambari 93, ikiwa
ni kumbukumbu ya bao lake la kipekee dhidi ya wapinzani wake Atletico Madrid
katika fainali ya Ligi ya Mabingwa 2013-14.
Hata hivyo, kulingana na mwandishi wa habari wa Bild Javi de
Hoyos, mke wa Ramos - mtangazaji maarufu wa TV Pilar Rubio - ameamua kusalia
Uhispania kwa 'sababu za kitaalamu'.
'Pilar Rubio hatahamia
Mexico na Sergio Ramos. Ijumaa iliyopita, mtu wa karibu na Pilar aliniambia
kuwa alikuwa amechoka kuhama,' alisema de Hoyos.
'Alikwenda Paris pamoja
naye, kisha Ramos akaenda Seville. Baadaye, aliamua kwenda Madrid kwa sababu za
kikazi. Anapenda sana kuishi huko.'
Rubio ni mwandishi maarufu wa Uhispania, mtangazaji wa
Runinga na mwanamitindo.
Uamuzi wake wa kubaki Uhispania unaweza kuhusishwa na ukweli
kwamba atashiriki kama jaji katika shindano la kila wiki la Antena 3, El
Desafio, na onyesho la uhalisia la mitindo la Maestros de la Costura.
De Hoyos aliongeza: "Wakati Pilar Ramos anafanya uamuzi
huu, alisema: "Safari hii sitakubali, tayari nimeshakubali mara mbili.
Sasa nabaki hapa, Madrid. Familia inabaki hapa, Sergio anaenda peke yake."
'Hawezi tena kuvumilia kulazimika kuhama tena.'
Wanandoa hao walianza uhusiano mnamo 2012 na kuolewa miaka
saba baadaye. Wana watoto wanne, Sergio Mdogo, Marco, Alejandro, na Maximo
Adriano.
Ramos amekuwa akipambana na majeraha mara kwa mara tangu
alipotoka bila kutarajia kutoka Real Madrid, ambapo alicheza mechi 671 huku
akifunga mabao 101.
Timu yake mpya Monterrey itakuwa miongoni mwa timu 32
zitakazoshiriki katika michuano ya Kombe la Dunia ya Klabu ya FIFA ya majira ya
kiangazi huko Marekani.
Watachuana katika Kundi E pamoja na River Plate, Urawa Red
Diamonds na Inter Milan.