
MWANAMKE mmoja ambaye ni mtengenezaji wa maudhui amezua gumzo kali katika mitandao ya kijamii baada ya video yake akilipia huduma kuoshwa kwenye kituo cha kuosha magari kusambaa mitandaoni.
Katika video hiyo, mwanamke huyo aliyekuwa amevalia rinda la
kahawia alielekea kwenye kituo cha kuosha magari ambapo aliwapata vijana wawili
wakiwa katika harakati za kuosha gari moja.
Kwa wakati huu wote, alikuwa anashikilia simu yake kwa mkono
mmoja huku akirekodi na kutumia mkono mwingine kuchomoa Burunguti la hela
kutoka kwa mfuko wake.
Kisha aliwauliza wale vijana wangemlipisha kiasi kipi kwa
huduma ya kumuosha kama vile gari, swali ambalo kwa sekunde kadhaa
liliwashangaza vijana wale.
Kisha baada ya kukubaliana bei, alimkabidhi mmoja wao hela na
kuwaamrisha wamuoshe kuanzia kichwa hadi wayo kwa sabuni na maji, mithili ya
gari – huku akirekodi tukio zima.
Vijana wale maadamu wameshapokea pesa, walianza mchakato wa
kumuosha kuanzia kichwani hadi miguuni huku Mrembo huyo alijirekodi licha ya
pofu jingi la sabuni kugubika uso wake.
Tukio hili lililizua mjadala mkubwa, huku wengi wakihoji hali
ya ubunifu katika kutengeneza skit.
Mcheshi maarufu wa Nigeria Klinton Cod alichapisha tena video
hiyo, akilaani kitendo hicho na kuwakosoa watengeneza maudhui wakuu kwa
kuidhinisha maudhui kama hayo.
Alisikitika kudorora kwa viwango vya ubunifu ndani ya tasnia hiyo na akapendekeza watayarishaji wa maudhui wasajiliwe na kupewa leseni ili kukabiliana na kile alichokitaja kuwa kero inayoongezeka.
Akikubaliana na maoni ya Klinton Cod, mtumiaji wa mitandao ya
kijamii @alsinasteve alijibu, "Tunapoteza maadili yetu tangu mitandao ya
kijamii ianze kuwalipa watu…wanaweza kufanya chochote kwa ajili ya pesa na
umaarufu."
Mtumiaji mwingine @justice_crack aliongeza, “Ninaamini
mapinduzi yanakuja katika tasnia ya uundaji maudhui. Ikiwa sote tutaendelea
kutangaza maudhui mabaya, tasnia yetu ya uundaji wa yaliyomo itabadilika na
kuwa bora kwa wakati.