
KIJANA kutoka India amevunja Rekodi ya Dunia ya Guinness kwa sura yenye nywele nyingi zaidi kwa mwanaume.
Lalit Patidar ana hali adimu inayoitwa
hypertrichosis, au 'werewolf syndrome' inayosababisha ukuaji wa nywele nyingi
usoni.
Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 18,
ambaye uso wake umefunikwa na nywele kwa 95%, anasema kuna wale ambao wanaweza
kuwa wasio na huruma kwake, lakini ameamua kukumbatia upekee wake.
Kwa mujibu wa jarida la Metro UK, Hivi
majuzi Lalit alisafiri kutoka nyumbani kwake katikati mwa jimbo la Madhya
Pradesh hadi Milan nchini Italia ili kupimwa idadi ya nywele zake kwa kipindi
cha TV cha 'Lo Show dei Record'.
Hilo lilihusisha kumtembelea mtaalamu wa
trichologist ambaye alinyoa sehemu ndogo za uso wake ili kuchukua vipimo sahihi
vya nywele zake kwa kila sentimeta ya mraba, kulingana na Guinness World
Records.
Kisha ikafunuliwa alikuwa na nywele
201.72 kwa kila cm ya mraba, na kumfanya rasmi kuwa 'Uso wenye Nywele Zaidi kwa
Mtu (Mwanaume)'.
"Lalit ni mojawapo tu ya visa
50 vilivyorekodiwa [vya hypertrichosis] vilivyoripotiwa ulimwenguni kote tangu
Enzi za Kati, na kumfanya kuwa mmoja kati ya watu bilioni,"
Guinness World Records ilisema kwenye tovuti yao.
Kijana huyo alisema ‘hakuwa na neno’ na
‘anafuraha sana’ kutambuliwa kama mshikilizi wa rekodi ya dunia.
Akizungumzia mitazamo ya watu kwake,
aliongeza: ‘Watu wengi ni wema kwangu. Inategemea mtu. Siku ya kwanza ya
shule haikuwa nzuri sana kwa sababu watoto wengine waliniogopa, lakini
waliponijua, walitambua kwamba mimi si tofauti sana nao.’
Baadhi ya watu wamemhimiza kunyoa nywele
za usoni, lakini alisema hana mpango wa kufuata ushauri wao.
‘Ninawaambia kwamba napenda jinsi
nilivyo na sitaki kubadilisha sura yangu,’
alieleza.