
WAZIRI wa mazingira katika kaunti ya Nairobi Geoffrey Mosiria kwa mara ya kwanza amezungumzia kiini cha ugomvi wake na mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino.
Akizungumza kwenye runinga ya NTV,
Mosiria alifichua kwamba bifu kati yake na Owino haijaanza wakiwa viongozi
katika nyadhifa tofauti kwenye kaunti ya Nairobi bali ni ugomvi ambao una
mizizi yake tangu wakiwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi.
Kulingana na Waziri huyo wa kaunti,
walianza kugombana na Babu Owino wakati wote walijikuta wakiwa washindani wa
wadhifa wa rais wa wanafunzi katika chuo cha Nairobi.
Hata hivyo, Babu Owino ambaye anajulikana
kuwa kiongozi wa wanafunzi chuoni Nairobi kwa muda mrefu alimshinda Mosiria,
uchaguzi ambao Waziri huyo wa kaunti anadai kwamba ulihitilafiwa kwa faida ya
Owino.
“Bifu yangu na Babu inarudi nyuma
hadi tukiwa chuoni, Babu anaamini kwamba Mosiria hawezi kumshinda. Niliwania dhidi
ya Babu Owino katika uchaguzi wa SONU (chuoni Nairobi) na kura ziliibwa kwa
faida ya Babu kwa sababu yeye alikuwa ni kibaraka wa uongozi wa chuo. Na bifu
hiyo bado ingalipo,” Mosiria alisema.
Mosiria alisema kwamba licha ya wote
kuondoka katika siasa za chuoni na kujipata katika njia tofauti katika uongozi
wa kaunti ya Nairobi, bado anahisi Owino anahisi kuwa yeye ni tishio kwake.
“Hapa sasa mimi ni afisa mkuu wa
mazingira ya kaunti chini ya gavana Sakaja na Babu ni mbunge Embakasi Mashariki.
Lakini bado anahisi kwamba mimi ni tishio kwake na pengine anahisi kwamba
huenda nitakata kuwania ubunge katika eneobunge lake.”
Afisa huyo wa mazingira hata hivyo
alimshauri Owino kutokuwa na wasiwasi anapomuona akifanya mashauriano na vijana
katika eneobunge lake wakati amezuru kufanya angalizo kuhusu uchafuzi wa
mazingira na kumtaka kuacha kuingilia utendakazi wa kaunti.
“Lakini ningependa kumwambia ndugu
yangu, hudumia watu wako kwa heshima na taathima, fany kazi ambapo Mungu
amekupa na achene kuingilia utendakazi wetu kama maafisa wa mazingira kwa
kuchapisha picha ambapo kuna takataka. Badala yake wewe kama kiongozi toa
suluhisho,” Mosiria alimaliza kwa kumshauri
Owino.