
HUKU visa vya uhalifu na mashambulizi ya majangili yakiendelea kuripotiwa katika Maeneo mbalimbali nchini Nigeria, gavana wa jimbo la Niger, Umar Bago ametoa amri ya kukamatwa na kunyolewa kwa mtu yeyote mwenye rasta.
Katika video iliyosambazwa mitandaoni ambapo alikuwa Akizungumza
katika mkutano wa usalama wa wadau uliofanyika katika Ikulu ya Serikali
Jumanne, gavana huyo alisema nywele za watu hao zinafaa kukatwa na kutozwa
faini.
"Hatutavumilia
ukatili wowote. Mtu yeyote utakayemkuta ana dreadlocks, mkamate, nyoa nywele na
mtoze faini.”
"Hakuna mtu
anayepaswa kubeba aina yoyote ya nywele ndani ya Minna. Nimetoa amri za
kuandamana kwa vyombo vya usalama," alisema.
Kwa mujibu wa jarida la PUNCH, Mkutano huo ulihudhuriwa na
vyombo vya usalama na watawala wa kimila.
Aliwataka wazazi kuwaonya watoto wao, akisema serikali
itaanza kutekeleza hatua kali za usalama.
"Wazazi wanapaswa
kuwaonya watoto wao. Kuanzia wakati huu, ni 100% ya kulipa moto kwa moto.”
"Pia, nyumba yoyote
itakayopatikana ikiwa na wahalifu inapaswa kubomolewa. Jimbo la Niger si la
watu wasio na manufaa," gavana Bago aliongeza.
Pia alitangaza vizuizi vya usafirishaji wa pikipiki za
kibiashara na tuktuk kati ya saa kumi na mbili jioni na saa kumi na mbili
asubuhi huko Minna, akibainisha kuwa ni zile tu zinazotumika kwa dharura za
matibabu ndizo zitaruhusiwa kuhudumu kwa muda wote.
Aidha mkuu huyo wa jimbo aliwaagiza viongozi wa mitaa, wakiwemo wakuu wa wilaya, vijiji na kata, kuhakikisha wanaweka kumbukumbu sahihi za wakazi katika jamii zao.
Aliongeza kuwa mali yoyote itakayotumika kuwahifadhi wahalifu
au kuuza dawa za kulevya itaharibiwa.