
Rais William Ruto amesema yuko tayari kukabiliana na wakosoaji wake kwenye debe mwaka 2027, akiongeza kuwa amefanikisha mengi kwa nchi hii kiasi cha kustahili muhula wa pili madarakani.
Rais alitoa kauli hiyo alipokutana na maaskofu, wachungaji na wainjilisti 500 kutoka Shirikisho la Makanisa ya Kiinjilisti na ya Asili ya Kiafrika katika Ikulu ya Nairobi siku ya Jumatano.
Rais Ruto alisema atabaki kushikilia ajenda ya mabadiliko ya nchi, akiongeza kuwa hakuna upinzani wa aina yoyote utakaomteteresha.
Alimnukuu aliyekuwa Rais wa Marekani Abraham Lincoln aliyesema: “Ukubwa wa kiongozi hupimwa na dhamira anayoiamini na sadaka anayokubali kuitoa ili kuifikia.”
Rais alisema hakuna kiwango chochote cha uongo kitakachoweza kuficha ukweli wa maendeleo ambayo nchi imepiga, akiongeza kuwa matokeo ni dhahiri kwa kila mmoja kuyaona.
Aidha, alisema wakosoaji wake hawana ajenda mbadala, badala yake huepuka hoja halisi na kujificha kwenye maneno ya kisiasa yasiyo na maana.
“Niko tayari kwa mtihani wa 2027. Nina ripoti thabiti ya mafanikio. Nitatoa hesabu ya kile nilichotekeleza,” alisema.
Rais alisema serikali imeweka mikakati mahsusi ya kuimarisha uchumi.
“Leo, naweza kusema uchumi wetu ni imara na tunasonga mbele,” alisema.
Rais alieleza kuwa mfumuko wa bei uliokuwa asilimia 9.6 mwaka 2022 umeshuka hadi asilimia 3.8, huku kiwango cha ubadilishanaji wa shilingi dhidi ya dola kutoka Ksh.165 kikistahimili na kubaki karibu Sh130 katika kipindi cha miezi 15 iliyopita.
Akiba ya dola katika Benki Kuu ya Kenya imeongezeka kutoka dola bilioni 7 mwaka 2022 hadi kufikia dola bilioni 10.8 kwa sasa.
Aliposhika hatamu za uongozi, Rais Ruto alisema Kenya ilikuwa miongoni mwa nchi sita za Afrika zilizoorodheshwa kuwa hatarini kushindwa kulipa madeni.
Katika sekta ya kilimo, Rais alisema serikali imewasaidia wakulima kwa kuwapatia mbolea kwa bei ya ruzuku, hatua iliyoongeza uzalishaji na tija.
Hili limepelekea kushuka kwa gharama ya bidhaa za msingi kama mahindi, ambapo bei ya pakiti ya kilo 2 imeshuka kutoka Ksh.240 hadi kati ya Ksh.100 na Ksh.160 kutegemeana na chapa.
Rais alisema serikali pia imekabiliana na matapeli katika sekta ya kahawa na hivyo kuhakikisha wakulima wanapata mapato bora.
“Walikuwa wakipata wastani wa Sh70 kwa kilo; sasa wanapata kati ya Ksh.110 na Ksh.150 kutegemeana na kiwanda,” alisema.
Kuhusu sekta ya miwa, Rais Ruto alisema mageuzi yaliyofanyika yamewezesha wafanyakazi na wakulima kulipwa kwa wakati na kwa mara ya kwanza kupata bonasi.
Alisema uzalishaji umeongezeka kutoka tani 500,000 mwaka 2023 hadi tani 800,000 mwaka jana, na mwaka huu unatarajiwa kufikia tani 900,000.
“Katika kipindi cha miaka mitatu, Kenya itakuwa muuzaji wa sukari nje ya nchi,” alisema.
Ili kuimarisha sekta ya elimu, alisema serikali imeajiri walimu 76,000 na inapanga kuajiri walimu wengine 24,000 mwishoni mwa mwaka huu. Ajira hizi 100,000 kwa kipindi cha miaka mitatu zitakuwa nyingi zaidi katika historia ya taifa hili.
Kuhusu mpango wa huduma ya afya kwa wote, Rais Ruto alisema ameazimia kuuendeleza kuhakikisha hakuna Mkenya anayeachwa nyuma au kulazimika kuuza mali ili kugharamia matibabu.
Rais alisema ataendelea kuwaunganisha Wakenya na kuwahamasisha kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya nchi.
Rais aliwakosoa wanaompinga kuhusu mpango wa kujenga kanisa Ikulu, akisema kuwa zaidi ya familia 300 zinaishi katika eneo hilo na kwa sasa huabudu kwenye jengo la mabati lenye hali duni sana.
“Hadithi mnasikia kuwa ujenzi wa kanisa utagharimu mabilioni ni lugha ya shetani ya kuwapotosha wananchi,” alisisitiza.
Aliwakumbusha Wakenya kuwa Kenya ni taifa linalomcha Mungu, msimamo ulioelezwa waziwazi katika Katiba.
Viongozi wa makanisa waliwakosoa wanaopinga ujenzi wa makanisa.