
NAIROBI, KENYA, Julai 26, 2025 — Mwanamuziki na mtangazaji mashuhuri nchini, Sanaipei Tande, ameweka wazi tukio la kushangaza alilokumbana nalo akiwa na umri wa miaka 21, muda mfupi baada ya kujiunga na redio ya Kiss 100 FM.
Katika mahojiano ya hivi majuzi, Sanaipei alieleza kuwa mtangazaji mkongwe Maina Kageni alimtolea ombi la ajabu: amzalie mtoto na kwa malipo hayo apewe maisha ya kifahari yasiyo na kazi.
"Maina aliniambia, "Usipotaka kufanya kazi tena maishani mwako, nipe tu mtoto," alisimulia Sanaipei.
Ombi hilo lilihusisha malipo ya kila mwezi ya KSh 500,000, nyumba katika mtaa wa kifahari wa Lavington, na ahadi nyingine kutoka kwa mama ya Maina ambaye aliahidi kumpatia mama wa mtoto huyo nyumba ya kifahari.
Sanaipei alisema kuwa wakati huo alikuwa hajaanzishwa kipindi chake binafsi na alikuwa bado anajifunza kazi ya utangazaji.
Ingawa baadhi ya ripoti zilidai alikuwa na umri wa miaka 22, alisisitiza kuwa alikuwa mchanga sana na hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mazingira ya tasnia hiyo.
"Nilikuwa bado mtoto. Nilijua nataka kujijenga kitaaluma kwa misingi yangu mwenyewe," alieleza.
Sanaipei alisema wazi kuwa hakuwahi kufikiria kuingia kwenye uhusiano wa aina hiyo, hasa katika kipindi ambacho alikuwa anajitahidi kujenga taaluma na jina lake binafsi.
"Pesa hazinidhibiti. Sitaki maisha ya starehe yaliyojaa masharti ya kihisia," alisema kwa msisitizo.
Licha ya mashinikizo kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii waliomsifia Maina na kumshauri akubali "fursa ya kipekee", Sanaipei alikataa kwa uthabiti, akisisitiza kuwa heshima na maamuzi ya kibinafsi hayawezi kuuzwa kwa fedha.
Maina baadaye alikiri hadharani kwamba alitoa ombi hilo, akieleza kuwa halikuwa la kimapenzi bali alitaka kuwa baba bila kuwa kwenye uhusiano wa moja kwa moja.
Wito kwa Wanawake Chipukizi
Sanaipei alitoa ujumbe maalum kwa wanawake vijana, hasa wanaoanza kazi kwenye tasnia ya burudani, kuzingatia kujijenga kitaaluma kabla ya kuchukua majukumu makubwa ya maisha.
"Jijenge kwanza kifedha, kitaaluma na kiakili kabla ya kuingia kwenye mambo yanayoweza kubadilisha maisha yako," alieleza.
"Usikubali starehe ya muda mfupi ikutose amani ya maisha ya baadaye."