
Kaka wa marehemu Betty Bayo, Edward Mbugua, ametoa kauli nzito akidai kuwa mwimbaji huyo wa injili hakuwahi kuolewa rasmi na Hiram Gitau, anayejulikana kama Tash, hatua ambayo imezua upya mjadala kuhusu urithi, malezi ya watoto na nafasi ya familia katika maamuzi yanayofuata msiba.
Wiki chache baada ya kumzika Bayo, Mbugua alianza kuchapisha video kwenye TikTok akidai kuwa familia yao imezuiwa kuingia katika makazi ya marehemu.
Mbugua Adai Hakukuwa Na Ndoa Kati Ya Bayo Na Tash
Mjadala uliwaka moto alipomjibu mtumiaji mmoja wa TikTok aliyedai kuwa kisheria, kama hakuna wosia, Tash angehesabika kama mrithi mkuu kwa kuwa ndiye mume wa marehemu.
Mbugua alikataa hoja hiyo moja kwa moja.
"Kila kitu kiko kwa next of kin, na sasa mambo yanaanza kuonekana. Hakukuwa na mtu aliyeolewa hapa. Haijawahi kufika hapo. Kilichofanyika ni sherehe tu. Kama mnajua desturi za ruracio, hakuna kitu kilifanywa na mimi nilikuwepo," alisema.
Kauli hii imeleta maswali mapya kuhusu hadhi ya uhusiano uliokuwa ukionekana hadharani kuwa wa ndoa.
Alisema hali ya mawasiliano kati yao na Tash ilidorora mara tu baada ya mazishi, jambo lililowaacha bila nafasi ya kuwa karibu na watoto.
Mbugua alisema walichotaka ni uwazi na haki.
"Kitu cha kwanza ni kwamba hatuna ufikiaji wa nyumba ya dada yangu. Hilo pekee linaumiza. Hatuwezi hata kuwaona watoto, na hiyo si haki," alisema.
Kwa Nini Anamtetea Pastor Kanyari
Katika ujumbe wake, Mbugua alimrejea sana Pastor Victor Kanyari, akimtaja kama mzazi wa kweli wa Sky na Danny.
Alisema kuwa licha ya tofauti zao za miaka iliyopita, Kanyari aliendelea kuwa kwenye maisha ya watoto.
"Kanyari ni baba wa damu wa Sky na Danny, na sisi tunashirikiana naye kama familia. Hawa ni watoto wetu, na hatuwezi kugawanywa kwa mali au majina ya watu," alisema.
Alisisitiza kuwa uhusiano wa kifamilia haupaswi kuvunjika kwa sababu ya hali za sasa.
Mali Za Bayo Na Mustakabali Wa Watoto
Akiendelea kueleza, Mbugua alisema miaka mingi amekuwa akifuatilia uwekezaji ambao dada yake alifanya, akisema mara kwa mara alimshirikisha katika mipango yake ya mali.
"Nataka kila kitu cha dada yangu kiwekwe sehemu moja kwa sababu watoto wanakua na hizo ndizo mali za mama yao. Hilo halina mjadala," alisema.
Kauli hii imezua mjadala mpana kuhusu sheria za urithi nchini, hasa pale ambapo hakuna wosia ulioandikwa.
Ukimya Wa Tash Wazidisha Tetesi
Hadi sasa, Tash hajatoa tamko lolote hadharani. Ukimya wake umezua hisia mseto, wengine wakimtaka aseme ukweli kuhusu hadhi ya ndoa, huku wengine wakimtetea kwamba masuala ya kifamilia hayapaswi kuamuliwa mtandaoni.
Mashabiki wamegawanyika, baadhi wakisema familia inapaswa kuketi mezani, wengine wakiona watoto ndio wanaohitaji utulivu zaidi.
Sheria Na Mila Zatatizwa Na Madai Haya
Wataalamu wa sheria wanasema kesi kama hizi huwa ngumu hasa pale ambapo mahusiano ya kimapenzi hayakuthibitishwa kwa hati ya ndoa au desturi kamili za kitamaduni.
Pindi kunapokosekana nyaraka au ushahidi wa ndoa, mahakama mara nyingi huamua kwa kuzingatia ushahidi wa mwenendo wa uhusiano.
Kwa upande wa urithi, wataalamu wanasema mambo huwa magumu zaidi pale ambapo kuna watoto kutoka uhusiano wa awali.
Utata huu, wakionya, unaweza kuwa na athari kubwa kwa ustawi wa Sky na Danny.
Hatua Zinaweza Kukwenda Mahakamani
Zaidi ya hisia zinazoendelea, wataalamu wanashauri usuluhishi wa kifamilia ili kulinda ustawi wa watoto.
Hata hivyo, uhalisia unaonyesha kuwa suala hili linaweza kuishia mahakamani kama pande husika hazitakubaliana kuhusu mali na malezi.
Kwa sasa, macho yameelekezwa kwa Tash na Pastor Kanyari. Wote wawili wana nafasi kubwa katika mustakabali wa watoto, lakini mwelekeo utategemea hatua watakazochukua katika siku zijazo.







© Radio Jambo 2024. All rights reserved