logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mgogoro wa Pesa Wavuruga Mapenzi ya Doris na Michael

Ukweli, Umaskini na Uaminifu

image
na Tony Mballa

Burudani07 January 2026 - 16:01

Muhtasari


  • Uhusiano wa Doris na Michael umefikia mwisho baada ya Michael kugundua kuwa Doris alipokea msaada wa pesa kwa siri kutoka kwa marafiki na jamaa wakati wa ugonjwa wa mtoto na mama yake, hali iliyozua lawama, kutoaminiana na tuhuma nzito.
  • Katika simulizi ya kugusa hisia, Doris anaeleza jinsi umaskini, hofu na shinikizo la kifamilia vilivyomsukuma kukubali msaada wa kifedha kwa siri, hatua ambayo Michael aliitafsiri kama usaliti, na hatimaye kuuvunja uhusiano wao wa miaka mitano waliokuwa wamejenga kwa jasho na subira.

Mwanamke aliyesongwa na mawazo

NAIROBI, KENYA, Jumatano, Januari 7, 2026 – Uhusiano wa miaka mitano kati ya Doris na mwenzi wake Michael umevunjika ghafla baada ya Michael kugundua kuwa Doris alipokea msaada wa kifedha kwa siri kutoka kwa rafiki wa kiume wakati wa nyakati ngumu, zikiwemo ugonjwa wa mtoto na maradhi ya mama yake.

Ugunduzi huo, uliofanyika mapema Januari kupitia rekodi za miamala ya simu, ulizua lawama nzito, kutoaminiana na mwisho wa uhusiano uliowazaa watoto wawili.

Uhusiano Uliojengwa kwa Jasho na Subira Doris anasema uhusiano wao haukuwa rahisi tangu mwanzo.

“Hatujafunga ndoa kisheria, lakini Michael alikuja kwa watu wangu,” Doris anasema. “Hiyo ni hatua kubwa sana kwetu.”

Anamwelezea Michael kama mtu mwenye bidii kubwa. “Alikuwa akifanya kazi za kila aina ili tu tupate chakula mezani,” Doris anasema. “Nilithamini sana juhudi zake.” Lakini juhudi pekee hazikutosha kuzuia dharura.

Mtoto Kuugua, Pesa Kukosekana

Chanzo cha kwanza cha mpasuko kilikuja mtoto wao alipougua. “Mtoto wangu alikuwa mgonjwa,” Doris anakumbuka. “Siku ya pili hakuna dawa, hakuna pesa.”

Akiwa hana pa kukimbilia, alimwomba jirani karibu na duka lake amkopeshe Sh3,000. “Nilikuwa na hofu,” Doris anasema. “Nilitaka tu mtoto wangu apone.”

Alipomweleza Michael, hali ilibadilika ghafla. “Alikasirika sana,” Doris anasema. “Alinizungumza vibaya.” Onyo alilopewa halikusahaulika. “Aliniambia nisiwahi kumuomba mtu yeyote msaada tena,” Doris anasema.

“Niliomba msamaha nikakubali.”

Ugonjwa wa Mama na Shinikizo la Kifamilia

Mwezi Desemba, mama yake Doris aliugua. “Mimi ni mzaliwa wa kwanza,” Doris anasema. “Majukumu yote yalielekezwa kwangu.”

Nyumbani hali ilikuwa mbaya. “Hatukuwa hata tunapata chakula cha kutosha,” anasema. Shinikizo kutoka kwa ndugu liliongezeka, likigeuka matusi.

“Walinitukana mimi na hata Michael,” Doris anasema. “Lakini sikumtaka anipe pesa.”

Akiwa na kumbukumbu ya onyo alilopewa, alichagua ukimya. “Niliita rafiki akanisaidia,” Doris anasema. “Sikumwambia Michael.”

Msaada Uliokuja Kwa Siri

Akiwa kijijini kumwona mama yake, Doris alikutana na rafiki wa zamani. “Nilimweleza kila kitu,” anasema.

Baadaye jioni, alipokea msaada mdogo. “Hakuniomba chochote,” Doris anasisitiza. “Alitaka tu kunisaidia.” Aliendelea kunyamaza.

Ahadi, Matumaini na Kimya

Alipokuwa akirejea mjini, Michael alipiga simu. “Aliniambia niwasalimie watu nyumbani,” Doris Anastasia.

“Akanitumia Sh5,000 ya nauli.” Krismasi ilipita bila msaada wowote. “Lakini tarehe 31 alinipigia,” Doris anasema.

Michael alimtumia Sh20,000. “Nilikua na furaha sana,” Doris anasema. “Nilihisi hakunisahau.” Siku chache baadaye, kaka yake mkubwa alimsaidia kwa Sh10,000. “Hakujua chochote,” Doris Anastasia.

Usiku Uliobadili Kila Kitu

Usiku mmoja akiwa amelala, Michael alichukua simu yake. “Aliangalia miamala yote,” Doris anasema. Kilichofuata kilikuwa moto.

“Kila kitu kiliharibika,” anasema. Michael alimtuhumu vikali. “Alisema hakuna mwanaume anayemtumia mwanamke pesa bila kulala naye,” Doris anasema.

Anakanusha madai hayo. “Mungu ni shahidi wangu,” Doris anasema. “Sikuwahi kulala na mtu kwa sababu ya pesa.”

Msamaha Usiokubalika

Doris anasema aliomba msamaha mara nyingi. “Nilimwambia onyo lake ndilo lililonifanya nifanye mambo kwa siri,” anasema.

Anasisitiza kuwa alichofanya kilikuwa kwa ajili ya kuokoa hali. “Nilikuwa na nafasi ya kusaidiwa,” Doris anasema. “Nilihitaji msaada.”

Lakini Michael hakuonyesha kulegeza msimamo. “Aliniambia hataki kuwa na mimi tena,” Doris anasema kwa huzuni.

Kwa Doris, mgogoro huu una mizizi kwenye umaskini. “Pesa zikikosekana, hofu huongea,” Doris anasema.

Anasema hakukaa kimya kwa sababu ya hatia. “Nilikaa kimya kwa sababu ya woga,” anasema.

Amani Ndani ya Nafsi

Licha ya maumivu, Doris anasema dhamiri yake iko safi. “Mama yangu alifanya makosa kwenye ndoa yake,” Doris anasema.

“Nilijifunza.” Anaamini ukweli wake unajulikana. “Moyo wangu ni safi,” Doris anasema. “Mungu anaona.” Na kwa sasa, hiyo inamtosha. “Hiyo peke yake inanitosha,” anahitimisha.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved