logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Akothee atoa onyo kali huku akitangaza mambo ambayo hataki yafanyike akifariki

Kufuatia kesi ya Brian Chira, mwimbaji huyo sasa amewaonya watu dhidi ya kumsherehekea wakati akikufa.

image
na Samuel Maina

Burudani24 March 2024 - 06:55

Muhtasari


  • •Mama huyo wa watoto watano alisema kwamba watu walipaswa kumsaidia marehemu alipokuwa angali hai.
  • •Kufuatia kisa cha Brian Chira, mwimbaji huyo sasa amewaonya watu dhidi ya kumsherehekea wakati akikufa.
Akothee

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amelalamika kuhusu  jinsi watu wanavyoonyesha upendo mwingi kwa Brian Chira baada ya kifo chake.

Akizungumza wakati wa kipindi cha moja kwa moja kwenye Tiktok, mama huyo wa watoto watano alisema kwamba watu walipaswa kumsaidia marehemu alipokuwa angali hai.

Alibainisha kuwa tayari Chira alikuwa ameomba usaidizi mara kadhaa lakini badala ya kumsaidia, watu walimdhihaki.

“Nimehuzunishwa sana na kifo cha kijana huyu. Mimi binafsi simfahamu, niliona video zake zikiibuka kulia, kushoto na katikati. Unapotazama video zake, alikuwa na roho ya furaha, alikuwa akijaribu tu kuishi. Maisha yake yalikatizwa,” Akothee alisema.

Msanii huyo alisema aliona video ya marehemu Chira akiomba usaidizi lakini hakumtafuta kumsaidia kwani alihofia matokeo ya usaidizi wake.

“Video ya mwisho niliyopatana nayo ni ile aliyosema anahitaji msaada, lakini kutokana na kuumizwa na watu wengi, niliogopa kumfikia. Kwa sababu nisingejua msaada wangu ungechukua mkondo gani,” alisema.

Aliongeza, “Hata hivyo, niliendelea kuomba apate msaada. Watu walimdhihaki. Unapotazama ndani kabisa ya video zake, kijana huyu alihitaji sana usaidizi. Nashangaa kwa nini nyote mnakimbia sasa ni kama mlijali mlijali kweli? Je, mko kutafuta kiki? Kwa nini watu maarufu wanakuwa maarufu zaidi wakiwa wamekufa, kwa sababu hakuna mtu anayetaka kushindana na maiti.”

Kufuatia kesi ya Brian Chira, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 sasa amewaonya watu dhidi ya kumsherehekea wakati akikufa.

"Sitaki mtu yeyote kuchangia siku yangu ya mazishi. Sitaki mtu yeyote anisaidie wakati nimekufa. Sitaki mtu yeyote kuposti picha zangu na wao wakati nimekufa. Chapisha picha hizo sasa. Niambie kila kitu ulichonacho cha kuniambia sasa nikiwa bado natembea. Usianze kuandika machapisho marefu ya jinsi nilivyokuhimiza, jinsi ulivyonijali wakati hukuwahi kuniambia mambo haya wakati wote, "alisema.

Aliendelea kuwashutumu wanamtandao kwa kutafuta kiki kutumia kifo cha mwanatiktok huyo na akaonya dhidi ya hilo kutokea wakati wa kifo chake.

"Nikiwa nimekufa na kuondoka, usiposti picha kwenye mitandao ya kijamii, wakati hujawahi kuposti picha za kuniambia mambo mazuri ambayo ningependa kusikia. Usiniambie ni kiasi gani ulinipenda wakati nimekufa na nimeenda, sitakusikiliza. Sijui kuzimu inaonekanaje, lakini inasikitisha jinsi watu wanavyofuatilia watu waliokufa," alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved