Muigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie ameweka wazi kuwa hana tatizo lolote na baba wa mtoto wake, Mulamwah.
Pia amefutilia mbali madai kwamba amekuwa akimnyima mchekeshaji huyo nafasi ya kumuona binti yao Keilah Oyando.
"Keilah Oyando anaendelea vizuri kabisa. Mimi na baba yake hatuna shida yoyote. Wako huru kuonana kwa wakati wowote (Mulamwah na Keilah," Sonnie alisema katika mahojiano na Nicholas Kioko.
Mama wa mtoto mmoja pia alidokeza kwamba binti huyo wao wa miezi 11 bado anaendelea kukua vizuri.
Aidha aliweka wazi kuwa anafurahia sana uzazi na kubainisha kuwa bintiye amekuwa kitulizo cha huzuni yake.
"Kila siku najifunza, inaendelea kuwa rahisi kila siku. Sio kama mwanzo wakati nilimpata Keilah, saa hii najua nifanye nini na nisifanye nini. Nafurahia, huyo mtoto anafanya nisahau vitu mingi sana. Nikiona kitu inanikula kichwa, naangalia tu mtoto wangu na nafurahia," Alisema.
Muigizaji huyo amekuwa akiishi na binti yake baada ya kutengana na mchekeshaji Mulamwah miezi kadhaa kabla ya kujifungua.
Siku za hivi majuzi hata hivyo amekuwa akijigamba kuhusu mahusiano mapya na kumuonyesha mpenzi wake wa sasa hadharani. Sonnie hata hivyo amekuwa akionyesha sehemu tu ya mpenziwe na kuficha sura yake.
"Niliamua na kusema wacha watu waone niko na furaha lakini wasione ni nani anafanya niwe na furaha. Hawahitaji kuona uso wake lakini niko na furaha sana," Alisema Sonnie.
Sonnie alifichua kuwa amekuwa akichumbiana na mpenziwe mpya kwa kipindi cha takriban miezi miwili tu.
Hata hivyo alidokeza kuwa yeye na mpenzi huyo wake mpya wamekuwa marafiki kwa muda mrefu.
"Tumekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka 10. Alikuwa nje ya nchi, alirudi miezi michache iliyopita," Alisema.
Muigizaji huyo alidai kuwa ataandaa karamu kubwa ya kufichua sura ya mpenzi wake katika siku zijazo.
"Anaihitaji. Nitatumia pesa kwa ajili yake. Nitafanya karamu ya kufichua sura yake. Watu wanahitaji kumuona," Alisema.