"Kuna kitu alinipea kwingine siwezi pata" Nadia Mukami azungumzia uhusiano wake na Arrow Bwoy

Muhtasari

•Nadia ambaye kwa sasa ako Marekani pamoja na Arrow Bwoy kwa ziara ya muziki amekiri kuwa ana mapenzi makubwa sana kwa mpenzi wake na hana nia ya kumuacha.

•Takriban wiki mbili zilizopita matendo ya wawili hao mitandaoni yaliibua uvumi kuwa ndoa yao ya kipindi kifupi ilikuwa imegonga mwamba.

Image: INSTAGRAM//NADIA MUKAMI

Malkia wa muziki wa kisasa Nadia Mukami amepuuzilia mbali uwezekano wake kutengana na kipenzi chake kipya msanii mwenzake Arrow Bwoy.

Nadia ambaye kwa sasa ako Marekani pamoja na Arrow Bwoy kwa ziara ya muziki amekiri kuwa ana mapenzi makubwa sana kwa mpenzi wake na hana nia ya kumuacha.

Mwanamuziki huyo amesema kuwa kuna kitu maalum ambacho alipata kwa Arrow Bwoy ambacho hakuwahi pata kwa mtu mwingine yeyote.

"Napenda Arrow sana. Kuna kitu alinipea kwingine siwezi pata" Mukami alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Msanii huyo ambaye ana umri wa miaka 24 alikuwa anamjibu shabiki wake mmoja aliyehofia kwamba angenyakuliwa na jamaa mwingine akiwa katika ziara yake Marekani.

Mwezi uliopita Nadia na Arrow Bwoy waliweka wazi uhusiano wao kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Wawili hao waliamua  kujiitokeza kwani haikuwa rahisi tena kwao kuendelea kujificha hadharani ilhali walikuwa wanachumbiana kwa ufiche.

Mukami alisema kuwa amehitimu umri ambapo anataka kuanza kutengeneza familia pamoja na mpenzi wake.

" Sio kiki! naona watu hawaamini kwani kwa muda.. Hata mimi nimeanza kuzeeka, nahitimu miaka 25 mwaka huu. Inafikia wakati fulani ambapo unataka tu kufurahia maisha pamoja na mtu na unataka kujenga maisha ya usoni na mtu. Watu hawaamini, ni sawa. Hatuwezi badiliha dhana za mtu kutuhusu" Nadia alisema.

Takriban wiki mbili zilizopita matendo ya wawili hao mitandaoni yaliibua uvumi kuwa ndoa yao ya kipindi kifupi ilikuwa imegonga mwamba.

Uvumi kuwa kitumbua kilikuwa kimeingia mchanga ulianza kuenea baada ya Nadia Mukami kuchapisha ujumbe wa kimafumbo  ambao uliibua hisia kuwa huenda hali sio shwari tena kati ya wawili hao.

Ujumbe wa Nadia uligusia suala la udanganyifu na ukosefu wa uaminifu kwenye uhusiano. 

"Makosa sio ajali. Kutokuwa mwaminifu na kudanganya sio makosa, ni chaguo la kujitakia. Acha kujitetea na neno 'kosa' wakati unapokamatwa" Ujumbe wa Nadia ulisoma.

Punde baada ya hayo wawili hao waliacha kufuatana kwenye mtandao wa Instagram, hatua ambayo sana sana huchukuliwa na watu ambao wamekosana.

Hata hivyo, siku chache baadae walianza kuonekana wakitumbuiza mashabiki wao pamoja Marekani na kupuuzilia madai kuwa walikuwa wametengana.