"Ringtone ni chokoraa!" Eric Omondi ajitolea kupatia Ringtone Apoko malazi kufuatia madai kwamba amefungiwa nyumba

Eric alisema kwamba ako tayari kumpatia Ringtone chumba kimoja cha malazi katika jumba lake la kifahari ambalo alionyesha hadharani hivi majuzi.

Muhtasari

•Omondi amedai kwamba Apoko amelazimika kuhamia katika eneo moja kando ya barabara ya Jogoo Road baada ya kufurushwa kutoka kwa jumba lake lililo katika mtaa wa Runda.

•Hata hivyo, hapo awali Apoko alipuuzilia mbali madai kwamba jumba lake lilifungwa baada ya kushindwa kulipa kodi.

Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji Eric Omondi amedai kwamba ana uhakika kwamba nyumba ya mwanamuziki Ringtone Apoko imefungwa.

Omondi amedai kwamba Apoko amelazimika kuhamia katika eneo moja kando ya barabara ya Jogoo Road baada ya kufurushwa kutoka kwa jumba lake lililo katika mtaa wa Runda.

Akiwa kwenye mahojiano na Warbit katika mtandao wa YouTube, Omondi alidai kwamba kwa sasa Ringtone anasaidiwa na malazi na marafiki wake.

"Ringtone ni chokoraa.. Kwa nyumba yake kuwekwa kifuli na kuna karatasi imebandikwa. Ringtone nyumba yake ilifungwa. Najua nyumba yake. Ni nyumba ya umma, imefungwa. Ringtone haishi Runda, anaishi Jogoo Road" Eric alisema.

Mchekeshaji huyo alisema kwamba ako tayari kumpatia Ringtone chumba kimoja cha malazi katika jumba lake la kifahari ambalo alionyesha hadharani hivi majuzi.

Kando na malazi, Omondi aliahidi kumpatia mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili chakula na kugharamia mahitaji yake mengine ya kimsingi kwa kipindi cha miezi mitatu anapoendelea kutafuta kazi.

"Ringtone hatujui huwa unafanya kazi gani, mimi huwa nafanya vichekesho. Nipigie simu tunajua ukweli nyumba yake ilifungwa na ikauzwa. Saa hii uko mitaani unaishi na marafiki. Nyumba yangu iko na vyumba 11 vya kulala. Kuja nikupatie chumba kimoja uoge na ukule kwa kipindi cha miezi mitatu. Miezi mitatu nitakupa WiFi ya bure, chakula cha bure na kitanda cha bure" Alisema Eric.

Hata hivyo, hapo awali Apoko alipuuzilia mbali madai kwamba jumba lake lilifungwa baada ya kushindwa kulipa kodi.

Alipokuwa  kwenye mahojiano na wanablogu katika hafla ya kuzindua albamu ya Daddy Owen siku ya Jumamosi, Ringtone alisisitiza kwamba bado anaishi Runda na hajafurushwa na yeyote.

"Kila soko iko na wazimu wengi. Ukienda kwa soko upate wazimu anaongea sio lazima ujibu. Kujeni kesho asubuhi muone kama siishi hapo. Karibuni chai kesho asubuhi.. mimi naendelea na maisha yangu kwa sababu yako kama yalivyokuwa. Majirani wangu hawajalalamika" Ringtone alisema.

Hivi majuzi uvumi ulienezwa sana mitandaoni kwamba mwanamuziki huyo alikuwa amefurushwa kutoka kwa nyumba yake ya kukodisha baada ya kushindwa kulipa kodi.