'Naweza kunyonyesha vizuri hata kama nilifanyiwa upasuaji wa kuongeza ukubwa wa matiti,' Vera Sidika aeleza

Muhtasari

•Vera amesema kwamba alifahamu fika kwamba siku moja angetamani kupata mtoto na kwa hivyo alichagua kufanyiwa upasuaji kwa mtindo ambao haungesababisha madhara katika uzazi wake.

•Mama huyo wa mtoto mmoja amesema kwamba tangu bintiye alipozaliwa siku ya Mashujaa Day matiti yake yamekuwa makubwa zaidi na mazito kutokana na wingi wa maziwa.

•Mwaka uliopita mwanasoshalaiti huyo alishangaza wengi alipofichua kwamba ilimgharimu takriban shilingi milioni mbili kufanyiwa upasuaji wa kuongeza matiti yake.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti mashuhuri Veronica Mungasia almaarufu kama Vera Sidika ameweka wazi kwamba anaweza kunyonyesha bintiye vizuri licha ya kuwa alifanyiwa upasuaji wa matiti.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram mpenzi huyo wa mwanamuziki Brown Mauzo ameeleza kuwa upasuaji ambao alifanyiwa kufanya matiti yake yawe makubwa zaidi haukuathiri uwezo wake wa kunyonyesha mtoto.

Vera amesema kwamba alifahamu fika kwamba siku moja angetamani kupata mtoto na kwa hivyo alichagua kufanyiwa upasuaji kwa mtindo ambao haungesababisha madhara katika uzazi wake.

"Ndio unaweza kunyonyesha hata kama ulifanyiwa upasuaji wa matiti. Kuna chaguo. Unaweza kuchagua mtindo ambao utakuruhusu kunyonyesha hapo baadae ama ule ambao hautakuruhusu kunyonyesha. Nilijua nitapata watoto baadae kwa hivyo nilichagua mtindo ambao ungeniruhusu kunyonyesha" Vera alieleza.

Mama huyo wa mtoto mmoja amesema kwamba tangu bintiye alipozaliwa siku ya Mashujaa Day matiti yake yamekuwa makubwa zaidi na mazito kutokana na wingi wa maziwa.

Vera amefichua kwamba bintiye Asia Brown alianza kunyonya kwa ustadi masaa machache tu baada ya kuzaliwa.

"Punde tu baada ya Asia kuja duniani, matiti yangu yamejaa maziwa, hata hatujui tufanye nini nayo. Woi. Yamekuwa makubwa na maziti. Binti yangu alianza kunyonya punde midomo yake ilipogusa titi langu, masaa machache baada ya kujifungua. Alinyonya kwa ustadi" Alisema Vera.

Mwaka uliopita mwanasoshalaiti huyo alishangaza wengi alipofichua kwamba ilimgharimu takriban shilingi milioni mbili kufanyiwa upasuaji wa kuongeza matiti yake.

Alipokuwa mjamzito baadhi ya wanamitandao walitilia shaka uwezo wake wa kunyonyessha baada ya kujifungua.

Alipokuwa kwenye mahojiano katika Jalango TV mwaka uliopita Vera alieleza kwamba aliamua kufanyiwa upasuaji ili kufanya mwili wake uwe sawia kwani hapo mbeleni alikuwa na makalio makubwa na matiti madogo, jambo ambalo halikumpendeza.

"Nilikuwa mkubwa lakini sikuwa sawia kwa hivyo nikaamua kuwa sawia na nikaongeza ukubwa wa matiti yangu, Angalau huwa sivai sidiria tena.. Ilinigharimu dola 20000 na nilifanyiwa Beverly Hills. Ni vizuri kwa sababu haiathiri uwezio wangu wa kunyonyesha" Vera lisema