"Tunataka kupata watoto wengi" Eric Omondi na Ayen wazungumza kuhusu mpango wao wa ndoa

Muhtasari

•Wawili hao walisema kuwa wanatazamia kupata angalau watoto nane pamoja ila wanatofautiana kuhusu idadi ya watoto wa kike ambao wangependa kupata.

•Omondi alisema kuwa anapenda watoto wa kike sana na ndio maana anatazamia kuwa na watoto wengi wa kike.

Image: INSTAGRAM

Mcheshi mashuhuri Eric Omondi amedai kwamba anatazamia kufunga ndoa na mshindi wa Wife Material Monica Ayen na kuishi naye kwa kipindi kirefu zaidi.

Walipokuwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, Omondi alisema kuwa anatazamia kuishi na mzaliwa huyo wa Sudan Kusini hadi uzeeni.

Mcheshi huyo amesema kuwa kulikuwa na mvuto mkubwa kati yake na Ayen punde tu walipopatana kwa mara ya kwanza.

"Ningependa kuwa na Ayen kwa kipindi kirefu. Tutazeeka pamoja. Tangu mara ya kwanza nilipomuona Ayen tulielewana vizuri. Hata watu pale kwa nyumba walikuwa wanashindwa vipi" Eric alisema.

Wawili hao walisema kuwa wanatazamia kupata angalau watoto nane pamoja ila wanatofautiana kuhusu idadi ya watoto wa kike ambao wangependa kupata.

"Tunataka kupata watoto wengi hapa Kenya.. Mimi ni mwalimu wa Sunday School. Napenda kufanya kazi na watoto. Tunatofautiana, mimi nataka watoto saba wa kike na mvulana mmoja" Omondi alisema.

Omondi alisema kuwa anapenda watoto wa kike sana na ndio maana anatazamia kuwa na watoto wengi wa kike.

Kwa upande wake Ayen alisema kuwa anatazamia kupata takriban watoto nane

"Ningependa watoto nane, wakipundua sana wawe watano. Nataka watoto, napenda watoto sana" Ayen alisema.

Siku chache zilizopita mcheshi huyo aliapa kuoa mshindi huyo wa onyesho la tatu la shoo ya Wife Material.

Omondi alitangaza kwamba mwanamitindo Ayen ndiye aliyenasa moyo wake kwani alitimiza yote aliyokuwa anatafuta kwa mke.

Baba huyo wa mtoto mmoja anayejulikana aliapa kufunga ndoa na Bi Monica na kuishi maisha yake yote pamoja na yeye kwenye dhiki na faraja

"Monica Ayen-Omondi. Hongera kwa kushinda moyo wangu. Hongera kwa kushinda shoo ya mwisho ya Wife Material. Naahidi kukupatia mapenzi yangu yote. Nitakuheshimu. Nitakuheshimu kwa utu wangu wote. Naahidi kukulinda. Siwezi kusubiri kuanzisha familia pamoja nawe. Siwezi subiri kupata watoto warembo na wewe. Wewe sio tu mwanamitindo bali una moyo mzuri. Unanikamilisha kipenzi. Unanikamilisha mpenzi wangu" Eric alitangaza.

Alishukuru taifa la South Sudan kwa kumpa malkia wa ufalme wake huku akiahidi kumlinda na kumpatia mapenzi yasiyoisha.