"Aliniita adui nambari moja, alitishia kunivunja niwe jivu" Lilian Ng'ang'a afichua vitisho vya Mutua

Muhtasari

•Lilian ambaye kwa sasa anachumbia mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani amedai kwamba gavana Mutua amekataa kabisa kusonga mbele na maisha yake licha ya mahusiano yao kufika kikomo mnamo mwezi Juni.

•Lilian amesema kwamba kuvunjika kwa uhusiano wao kumeathiri gavana huyo sana na kutokana na hayo amekuwa akimpa vitisho pamoja na walio karibu naye.

•Lilian amesema kwamba Mutua alimtishia kuwa tayari kuna watu ambao wamejipanga kumuangamiza pamoja na marafiki wake.

Lilian Ng'ang'a na wakili wake Philip Murgor
Lilian Ng'ang'a na wakili wake Philip Murgor
Image: MERCY MUMO

Miezi michache baada ya kutangaza kutengana kwao, Lilian Ng'ang'a amevunja kimya kuhusu uhusiano wake wa sasa na aliyekuwa mpenzi wake gavana Alfred Mutua.

Lilian ambaye kwa sasa anachumbia mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani amedai kwamba gavana Mutua amekataa kabisa kusonga mbele na maisha yake licha ya mahusiano yao kufika kikomo mnamo mwezi Juni.

Alipokuwa anahutubia waandishi wa habari siku ya Alhamisi, Lilian alifichua kwamba gavana Mutua amekuwa akimhangaisha tangu walipotengana.

Lilian ameweka wazi kuwa Mutua hajatimiza ahadi ambayo alitoa walipokuwa wanatangaza kutengana kwao mwezi Agosti kwamba wangeendelea kuwa marafiki wazuri.

"Nilitamatisha uhusiano wangu na Alfred Mutua mwezi Juni mwakani. Mara kadhaa haswa wiki katika kipindi cha wiki mbili zilizopita  nimeona Mutua akisema kwa gazeti na mitandaoni kuwa sisi ni marafiki na eti uhusiano wetu ulitamatika kufuatia maafikiano ya pamoja. Huo ni uongo wake wa kawaida. Hatujazungumza naye tangu mwishoni mwa mwezi Agosti" Lilian amesema

Lilian amesema kwamba kuvunjika kwa uhusiano wao kumeathiri gavana huyo sana na kutokana na hayo amekuwa akimpa vitisho pamoja na walio karibu naye.

Bwana Mutua ameguswa sana na kutengana kwetu. Ingawa nilisema nataka kusonga mbele na maisha yangu, alifikiria vingine" Lilian amesema.

Amedai kwamba  Mutua tayari  amepiga hatua ya kuchukua baadhi ya mali ambayo ilikuwa imeandikiishwa kwa jina lake ikiwemo gari na hisa za hoteli.

Lilian amesema kwamba mgombeaji huyo wa kiti cha urais mwaka ujao anatazamia kuchukua kila kitu anachomiliki huku tayari akiwa amemwagiza arejeshe  pesa zote ambazo aliwahi kumpatia ama kutumia juu yake.

"Nilimuomba tumwe na utengano mzuri na nikamkumbusha kwamba hatukuwa tumefunga ndoa. Mutua aliniita adui nambari moja, alitishia 'kunivunja niwe jivu' akichukua kila kitu nilicho nacho na ninachomiliki. Kusema kweli tayrai ameanza kwani ameambia mawakili wake waagize pesa zote ambazo amewahi kunipatia ama kuidhinisha itumike juu yangu" Lilian amesema.

Kando na hayo gavana Mutua anadaiwa kutishia maisha ya mpenzi huyo  wake wa zamani pamoja na watu walio karibu naye.

Lilian amesema kwamba Mutua alimtishia kuwa tayari kuna watu ambao wamejipanga kumuangamiza pamoja na marafiki wake.

"Alisema kuwa kuna watu wamejitolea kuua watu walio karibu nami na akatishia kuwa huenda akakubali  ili apatie baadhi yao funzo. Kwa dharau alisema kuwa yeye ni mtu wa maana sana nchini na anaweza fanya chochote alichokuwa amepanga kunifanyia pamoja na marafiki wangu na asiadhibiwe. Alisema kuwa kuna watu ambao wako tayari na wamesubiri kunimaliza pamoja na marafiki wangu" Lilian amesema.

Amesema kwamba mnamo Okotoba 7 alipiga hatua ya kuenda mahakamani kuomba agizo ya kumzuia mwanasiasa huyo kwa kuwa alihofia kwamba maisha yake yamo hatarini.

Mpenzi huyo wa Juliani amesema kwamba gavana Mutua ametoa madai ya uongo kuwa yeye ni mtumizi wa mihadarati na anatumiwa na maadui wake wa siasa kumuangusha kisiasa.

"Mutua amenishtumu kuwa mtumizi wa madawa ya kulevya  na eti natumiwa na gavana Kibwana (ambaye ni mjomba wake) na mheshimiwa Kalonzo Musyoka kumuangusha kisiasa. Huo ni upuzi kwani sijawahi kuzungumza nao kibinafsi" Lilian amesema.

Lilian ameweka wazi kwamba  hakuwa mke wala mpenzi wa Mutua ila walikuwa washirika wa muda mrefu tu.

Amemwagiza gavana huyo arejeshe mali yake, aache kumtishia pamoja na wali karibu naye na kumsihi asonge mbele na maisha yake.

Hali kadhalika ameomba Inspekta Jenerali wa polisi na DPP waingilie kati na waidhinishe kuharakishwa kwa uchunguzi  na kushtakiwa kwa Mutua kwa uhalifu ambao amemtendea.