Eric Omondi afunguka kuhusu kutengana kwake na aliyekuwa mpenzi wake Chantal Grazioli

Muhtasari

•Omondi aliweka wazi kwamba hakukosana na malkia huyo ila kutenga kwao kulikuwa maafikiano ya pamoja.

• Alisema kwamba mpenzi huyo wake wa zamani alikuwa anatamani sana kufanya kazi kwa ndege na hukutaka kukatiza ndoto zake.

Eric Omondi na Chantal Grazioli
Eric Omondi na Chantal Grazioli
Image: ERIC OMONDI SOCIAL

Mchekeshaji Eric Omondi amefunguka kuhusu mahusiano yake na mpenzi wake wa zamani  Chantal Grazioli. 

Alipokuwa kwenye mahojiano katika Jalang'o TV siku ya Alhamisi, Omondi aliweka wazi kwamba hakukosana na malkia huyo ila kutenga kwao kulikuwa maafikiano ya pamoja.

Mchekeshaji huyo ambaye amekuwa akivuma sana mitandaoni hivi karibuni amefichua kwamba alitengana na Muitaliano huyo kwa sababu za kikazi.

Omondi alieleza kwamba Chantal alilazimika kuondoka Kenya kuenda Dubai kupata mafunzo ya kazi aliyokuwa amepata na kampuni ya huduma za ndege ya  Emirates.

"Chantal alipata kazi katika kampuni ya Emirates. Alikuwa mdogo sana. Unapopata kazi Emirates lazima uende Dubai miezi nane. Hakuna likizo lakini waweza pumzika kidogo pale Dubai.  Aliambia mama yake kwamba amepokea barua ya kazi, nilikuwa nimemsaidia kuwasilisha ombi. Shangazi yake mmoja akamuuliza anaenda Dubai aache mume wake na nani. Akanipigia akaniambia kuwa shangazi yake alikuwa amedai hawezi funga safari ya kuenda Dubai kwani atakuwa ameniacha pekee yangu" Omondi alisimulia.


Alisema kwamba wakati alipokuwa anapokea habari hizo alikuwa katika kaunti ya Meru kwa ziara ya kikazi.

Chantal alipoomba ushauri wa Omondi kuhusiana na suala lile mchekeshaji huyo alishiriki mazungumzo na nafsi yake na akaonelea ni vyema asimzuie mwanadada huyo kuanza kujijenga maisha bora ya usoni.

"Alikuwa na miaka 20. Mimi nilikuwa na miaka 35. Nilikuwa naishi maisha yangu vizuri na nilikuwa nimefanikisha ndoto zangu. Nilikuwa nafanya kazi ambayo niliishi kutamani, alafu yeye alikuwa msichana mdogo mrembo na tulikuwa tunatumia sababu eti "unaacha bwanako". Aliniuliza afanye nini. Aliuza kama abadilishe safari nikamwambia aende Dubai akachukue kazi hiyo mara moja" Omondi alisema.

 Alisema kwamba mpenzi huyo wake wa zamani alikuwa anatamani sana kufanya kazi kwa ndege na hukutaka kukatiza ndoto zake.

"Nilimwambia nenda ukirudi utanipata. Niliambia akienda na aende kabisa ni sawa lakini akirejea atanipata" Alisema.

Hata hivyo amefichua kwamba kwa sasa Chantal anaishi na baba yake katika mtaa wa Westlands jijini Nairobi.