"Alisema nitazaa kama kuku!" Vera Sidika afichua Brown Mauzo anadai mtoto wa pili sasa

Muhtasari

•Mwanasoshalaiti huyo amesema Mauzo anataka kumpachika ujauzito mwingine kwani alishangazwa sana na jinsi ilivyokuwa rahisi kwake kubeba ujauzito na kujifungua.

•Vera pia amesema mamake amependezwa sana na mjukuu wake  huku akidai kwamba amekuwa akijaribu kumchukua akae naye.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Takriban wiki tatu tu baada ya wanandoa Vera Sidika na Brown Mauzo kukaribisha mtoto wao wa kwanza duniani tayari wameanza kuwa na majadiliano kuhusu kupata mtoto wa pili.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vera amefichua kwamba tangu alipojifungua mtoto wa kike mnamo Oktoba 20 mumewe amekuwa akimshawishi wapate mtoto mwingine.

Mwanasoshalaiti huyo amesema Mauzo anataka kumpachika ujauzito mwingine kwani alishangazwa sana na jinsi ilivyokuwa rahisi kwake kubeba ujauzito na kujifungua.

"Kwa kweli mimi na mpenzi tumekuwa tukizungumza kuhusu kupata mtoto mwingine. Kusema kweli huwa ananiambia hivo kila siku. Alisema nitazaa kama kuku. Jamaa aliona ilivyokuwa rahisi kwangu na hakuamini. Hakuna aliyenitunza kama mgonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji kwa sababu ilikuwa kawaida tu kwangu"  Vera amesema.

Wapenzi hao wawili walibarikiwana binti, Asia Brown siku ya Mashujaa Day.

Alipokuwa anatangaza habari kuhusu kujifungua kwake, Vera alisema kwamba binti yao ataishi kuwa miujuza ambayo itakamilisha maisha yake na mumewe mwanamuziki Brown Mauzo.

"Tarehe 20.10.2021 mida ya saa nne na dakika 21 asubuhi, mtoto wa malkia alizaliwa. Asia Brown @princess_asiabrown. Utaishi kuwa miujiza ambayo itafanya maisha yetu yawe kamili" Vera alitangaza.

Siku chache kabla yake kujifungua, Vera alipuuzilia mbali madai kuwa anajuta kupachikwa ujauzito na mwanamuziki Brown Mauzo.

Vera alisema walikuwa wamepangia ujauzito huo na kudai kuwa alitazamia kubeba ujauzito mwingine punde baada ya kujifungua kifungua mimba chake.

"Vile tuko hapa tunafikiria kuhusu mtoto wa pili punde baada ya Mungu kutujalia binti wetu, Inshallah, na tena mtoto wa tatu na wa nne pamoja na mwanaume mmoja, mume wangu. Halafu kuna watu wanataka kusema eti najuta, LMAOOO. Huwa sifanyi makosa. Huwa napanga maisha yangu yote" Vera alisema

Mwanasoshalaiti huyo pia amesema mamake amependezwa sana na mjukuu wake  huku akidai kwamba amekuwa akijaribu kumchukua akae naye.

Amesema kuwa mama yake amekuwa akijaribu namna zozote atakavyoweza kumshawishi akubali kumkabidhi mtoto wake amsaidie kulea.

"Mama yangu amekuwa akifanya zaidi tangu siku ya kwanza.Ananipikia kila siku na kunitunza vizuri. Lakini ni mtego. Anampenda Asia sana na najua atamharibu sana na amchukue kutoka mikononi mwangu" Vera amesema.

Hata hivyo amesisitiza kuwa hatamruhusu hilo lifanyike kwa kuwa anahofia siku moja huenda bintiye akamuita kwa jina lake badala ya kumuita mama.