"Bahati aliiba nyota yangu!" Ringtone amshtumu Bahati kwa kutumia nguvu za uchawi dhidi yake

Diana alitimiza miaka 32 siku ya Ijumaa.

Muhtasari

•Ringtone alidai Bahati alimualika katika sherehe zile kwa kuwa alijihisi mpweke na anamhitaji sana ili maisha yake yaweze kuendelea vizuri.

•Apoko alimshutumu Bahati kwa kutumia jina lake kutafuta kiki na kutumia nguvu za uchawi kukabiliana naye.

•Apoko alisema Bahati amelemewa kutunza mke wake huku akidai kwamba siku hizi mama huyo wa watoto watatu ameparara sana na anarudiarudia mavazi.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Wikendiiliyopita mwanamuziki Kelvin Kioko almaarufu kama Bahati alifanyia mkewe Diana Marua sherehe kubwa  ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na kikundi kidogo cha wageni waliokuwa wamealikwa ikiwemo marafiki wa Diana na Bahati pamoja na wasanii mashuhuri nchini. 

Kati ya wasanii waliokuwa wamealikwa kwenye sherehe hizo ni pamoja na mwenyekiti wa kujibandika wa muungano wa wanamuziki wa Injili, Ringtone Apoko ambaye aliamua kukaidi maelezo ya sherehe  ya kuvaa nguo nyeupe na badala yake akaamua kuvaa kanzu nyekundu.

Ama kweli asante ya punda ni mateke, baada ya sherehe hizo kutamatika mwanamuziki huyo aliyezingirwa na drama nyingi katika taaluma yake aliamua kushambulia aliyekuwa amemualika kwenye sherehe.

Alipokuwa anahutubia wanahabari baada ya sherehe, Ringtone alidai Bahati alimualika katika sherehe zile kwa kuwa alijihisi mpweke na anamhitaji sana ili maisha yake yaweze kuendelea vizuri.

"Maisha yake haiwezi endelea vizuri bila kuniita. Ako mpweke na hana ndugu mwingine ambaye anaweza ita. Tena mimi ndiye mhubiri pekee maishani mwake, wahubiri wengine wote walimkataa. Mimi ndiye najaribu kumrudisha kwa Mungu. Ni kazi ngumu lakini Mungu ananisaidia" Ringtone alisema.

Mwanamuziki huyo aliyekuja kutambulika zaidi kutokana na kibao chake 'Pamela'  alimshutumu Bahati kwa kutumia jina lake kutafuta kiki na kutumia nguvu za uchawi kukabiliana naye.

"Kwa wakati mwingine muziki unalemea Bahati anaanza kuniingilia. Anapenda kutafuta kiki na jina langu. Asiponitaja kama huu wimbo wake haungevuma bila kunitaja. Juzi niliambiwa na mchungaji kuwa ile siku Bahati alinigonga tukiwa kwa jukwaa alikuwa anaiba nyota yangu. Alikuwa anatumia uchawi kunigonga ndiyo achukue upako wangu. Aliiba nyota yangu. Lakini uzuri tumekuwa kwa maombi na nyota yangu haiwezi potea. Aliambiwa na mganga ati akiwa jukwaani akinigonga ama ajaribu kuniguza  atachukua nyota yangu lakini hakuweza" Apoko alisema.

Isitoshe, Apoko alisema Bahati amelemewa kutunza mke wake huku akidai kwamba siku hizi mama huyo wa watoto watatu ameparara sana na anarudiarudia mavazi.

"Bahati watu wanalalamika eti Diana ameanza kuparara, anarudia viatu. Tafadhali tia bidii zaidi. Watu wanasema eti ile gari alinunulia Diana anaitumia sana. Kama huna pesa za gari kuja uniombe nitakusaidia" Ringtone alisema.

Diana alitimiza miaka 32 siku ya Ijumaa.