"Eric Omondi ndiye mchekeshaji fukara zaidi nchini!" Ringtone Apoko adai

Apoko alidai kuwa Eric Omondi ndiye mchekeshaji fukara zaidi nchini

Muhtasari

•Mwenyekiti huyo wa muungano wa wanamuziki wa nyimbo za injili wa kujibandika alidai kwamba Omondi ni ombaomba huku akimshtumu kutumia jina la wanamuziki kujenga taaluma yake.

•Apoko pia alimkemea mchekeshaji huyo kwa kumdhalilisha hapo awali akidai madai kuwa alifurushwa kutoka kwa nyumba yake iliyo Runda baada ya kushindwa kulipa kodi.

Ringtone Apoko, Eric Omondi
Ringtone Apoko, Eric Omondi
Image: INSTAGRAM

Mzozo kati ya mchekeshaji Eric Omondi na mwanamuziki Ringtone Apoko hauonekani kuisha hivi karibuni.

Masaa machache tu baada ya Omondi kuwashambulia wanamuziki wa Kenya akidai kuwa wameisha, wamezembea  na wanachosha, Apoko sasa ameamua kumjibu.

Alipokuwa anazungumza na wanahabari katika sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Diana Marua, Apoko alidai kuwa Eric Omondi ndiye mchekeshaji fukara zaidi nchini.

Mwenyekiti huyo wa muungano wa wanamuziki wa nyimbo za injili wa kujibandika alidai kwamba Omondi ni ombaomba huku akimshtumu kutumia jina la wanamuziki kujenga taaluma yake.

"Eric Omondi hafai kukaa katika meza ya wasanii. Anaweza kuwa tu mcheza densi wetu. Yeye pamoja na waachekeshaji wengine ambao wanajaribu kuwa kama sisi ni wacheza densi. Wengi wamekuwa wakitoa vichekesho juu yetu ndio wajulikane.  Eric Omondi ako na wafuasi lakini hana pesa. Butita anashinda Eric Omondi. Mammito anashinda Eric Omondi.  Yeye ndiye maskini kabisa. Ukiangalia ameendesa gari moja kwa miaka 15. Hana pesa za kununua gari nyingine. Mimi naendesha gari kubwa. Eric Omondi anaendesha gari mzee inazima kila siku.Yeye lazima aombe. Jimi Wanjigi alimsaidia gari.  Sisi wasanii tunafanya kazi, tunanunua magari yetu hatusbiri kupewa zawadi" Apoko alisema.

Apoko pia alimkemea mchekeshaji huyo kwa kumdhalilisha hapo awali akidai madai kuwa alifurushwa kutoka kwa nyumba yake iliyo Runda baada ya kushindwa kulipa kodi.

Alidai kwamba mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na drama anajaribu tu kushindana naye huku akisema kuwa hajafikia kiwango cha kutambuliwa kama msanii bora.

"Eric Omondi ni malkia wa drama. Yeye kazi yake  drama tu. Juzi alisema naishi Jogoo Road. Alijaribu kumaanisha mimi naishi mahali pabaya. Nilibaki kwa nyumba nikijiuliza kwani Jogoo Road kunaishi wanyama. Jogoo Road kunaishi watu wa Mungu. Yeye anataka kuwa kama mimi" Apoko alisema.

Haya yanajiri takriban wiki mbili tu baada ya Omondi kudai kuwa Apoko amelazimika kuhamia katika eneo moja kando ya barabara ya Jogoo Road baada ya kufurushwa kutoka kwa jumba lake lililo katika mtaa wa Runda.

"Ringtone ni chokoraa.. Kwa nyumba yake kuwekwa kifuli na kuna karatasi imebandikwa. Ringtone nyumba yake ilifungwa. Najua nyumba yake. Ni nyumba ya umma, imefungwa. Ringtone haishi Runda, anaishi Jogoo Road" Eric alisema

Eric alisema alikuwa tayari kumpatia Ringtone chumba kimoja cha malazi katika jumba lake la kifahari ambalo alionyesha hadharani hivi majuzi.

Kando na malazi, Omondi aliahidi kumpatia mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili chakula na kugharamia mahitaji yake mengine ya kimsingi kwa kipindi cha miezi mitatu anapoendelea kutafuta kazi.

"Ringtone hatujui huwa unafanya kazi gani, mimi huwa nafanya vichekesho. Nipigie simu tunajua ukweli nyumba yake ilifungwa na ikauzwa. Saa hii uko mitaani unaishi na marafiki. Nyumba yangu iko na vyumba 11 vya kulala. Kuja nikupatie chumba kimoja uoge na ukule kwa kipindi cha miezi mitatu. Miezi mitatu nitakupa WiFi ya bure, chakula cha bure na kitanda cha bure" Alisema Eric.