Chantal Grazioli aghadhabiswa na madai ya aliyekuwa mpenzi wake, Eric Omondi kuhusu walivyotengana

Muhtasari

•Chantal amekubaliana na Omondi kwamba utengano wao ulikuwa mzuri huku akiweka wazi waliafikia uamuzi wa kutengana kama watu wazima.

•Mwanamitindo huyo amesema hakuridhishwa na baadhi ya madai ambayo Omondi alitoa siku ya Alhamisi haswa kumhusu pamoja na familia yake. 

•Omondi alidai  Chantal alilazimika kuondoka Kenya kuenda Dubai kupata mafunzo ya kazi aliyokuwa amepata na kampuni ya huduma za ndege ya  Emirates.

Eric Omondi na Chantal Grazioli
Eric Omondi na Chantal Grazioli
Image: ERIC OMONDI SOCIAL

Siku chache baada ya  Eric Omondi kufunguka kuhusu mahusiano yake na mpenzi wake wa zamani Chantal Grazioli, malkia huyo amejitokeza kulalamika kuhusu baadhi ya madai ya mchekeshaji huyo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Chantal amekubaliana na Omondi kwamba utengano wao ulikuwa mzuri huku akiweka wazi waliafikia uamuzi wa kutengana kama watu wazima.

Hata hivyo mwanamitindo huyo amesema hakuridhishwa na baadhi ya madai ambayo Omondi alitoa alipokuwa kwenye mahojiano katika Jalang'o TV siku ya Alhamisi haswa kumhusu pamoja na familia yake. 

"Mimi sio mtu wa kutafuta kiki, nimekuwa nimenyamaza na sijawahi kuzungumza kuhusu mahusiano yangu ya zamani na Eric, tuliachana vizuri kama watu wazima. Ningependa kusafisha jina langu kutoka kwa wazimu huu, kuna mambo kunihusu  katika mahojiano ya hivi karibuni ambayo si ya kweli kunihusu pamoja na familia yangu" Chantal aliandika.

Amesema kuna watu ambao wamekuwa wakimhoji kuhusu madai ya Omondi huku akitoa ombi kwa wanaomtafuta wamuache ashughulikie maisha yake kwa amani.

" Kuna watu wamenitafuta wakiuliza kuhusu  madai ya uwongo ambayo yalitolewa kwa niaba yangu huku nje. Tafadhali niko na maisha yangu na biashara ya kuangazia kwa amani. Nitaendelea kushirikiana na watu serious pekee! Kwa watu wote wasio wakweli (mnajijua) wacheni kunipigia" Alisema Chantal.

Hata hivyo hakufichua ni madai ya Omondi yapi haswa ya ambayo hayakuwa ya kweli.

Alipokuwa kwenye mahojiano wiki jana, Omondi aliweka wazi kwamba hakukosana na malkia huyo ila kutenga kwao kulikuwa maafikiano ya pamoja.

Omondi alidai  Chantal alilazimika kuondoka Kenya kuenda Dubai kupata mafunzo ya kazi aliyokuwa amepata na kampuni ya huduma za ndege ya  Emirates.

"Chantal alipata kazi katika kampuni ya Emirates. Alikuwa mdogo sana. Unapopata kazi Emirates lazima uende Dubai miezi nane. Hakuna likizo lakini waweza pumzika kidogo pale Dubai.  Aliambia mama yake kwamba amepokea barua ya kazi, nilikuwa nimemsaidia kuwasilisha ombi. Shangazi yake mmoja akamuuliza anaenda Dubai aache mume wake na nani. Akanipigia akaniambia kuwa shangazi yake alikuwa amedai hawezi funga safari ya kuenda Dubai kwani atakuwa ameniacha pekee yangu" Omondi alisimulia.

Mchekeshaji huyo alisema Chantal alipomuomba ushauri kuhusiana na suala lile alishiriki mazungumzo na nafsi yake na akaonelea ni vyema asimzuie mwanadada huyo kuanza kujijenga maisha bora ya usoni.

"Alikuwa na miaka 20. Mimi nilikuwa na miaka 35. Nilikuwa naishi maisha yangu vizuri na nilikuwa nimefanikisha ndoto zangu. Nilikuwa nafanya kazi ambayo niliishi kutamani, alafu yeye alikuwa msichana mdogo mrembo na tulikuwa tunatumia sababu eti "unaacha bwanako". Aliniuliza afanye nini. Aliuza kama abadilishe safari nikamwambia aende Dubai akachukue kazi hiyo mara moja" Omondi alisema.

 Alisema mpenzi huyo wake wa zamani alikuwa anatamani sana kufanya kazi kwa ndege na hukutaka kukatiza ndoto zake.

"Nilimwambia nenda ukirudi utanipata. Niliambia akienda na aende kabisa ni sawa lakini akirejea atanipata" Alisema.

Alidai kuwa kwa sasa Chantal anaishi na baba yake katika mtaa wa Westlands jijini Nairobi.