Hatimaye mwanamuziki mashuhuri kutoka Tanzania Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize ametambulisha mpenzi wake mpya hadharani baada ya kukaa kipindi cha takriban nusu mwaka bila mchumba.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, nyota huyo wa Bongo amemtambulisha Briana kama malkia mpya kwenye ufalme wake huku akidai amekuwa akisubiri sana kueleza dunia jinsi anavyomthamini.
Katika tangazo lake Harmonize ameahidi kumpenda na kumlinda mwanadada huyo mrembo kweli anayeaminika kuwa na asili ya Australia.
"Nimekuwa nikingoja wakati huu kuaambia kila mtu kuwa anachomaanosha maishani mwangu ...!!!! Nataka kusema tu nakupenda sana maishani na Heshimu Kila Mwanamke...!!!! Kama dada❤ Rafiki ❤ Shangazi ❤ mama ❤ Naahidi kuwa hapo Kwa Ajili yako milele ⏲️ KARIBU KWENYE MY WORLD QUEEN (B) @briana__tz 👸" Harmonize aliandika huku akiambatanisha ujumbe huo na picha za mpenzi wake.
Siku za hivi karibuni wawili hao wamekuwa wakionekana pamoja katika maeneo mbalimbali ya burudani nchini Marekani ambako Harmonize amekuwa kwa muda katika ziara ya kimuziki.
Hivi majuzi Harmonize aliandika ujumbe ambao uliashiria kuwa kuna mwanadada ambaye ameunasa moyo wake na sasa anaogelea katika dimbwi la mapenzi.
"Hatimaye nina mwanamke wa maisha yangu," Aliandika Harmonize kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Hayawi hayawi hatimaye huwa, basi sasa staa huyo ameamua kufungua roho na kuweka wazi kuwa hayuko single tena kwani kapatamalkia wa kujigamba naye.