"Mimi ni Ex asiye na matatizo!" Hamisa Mobetto akana madai kwamba anajaribu kumkomoa Diamond

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili alisema huwa hafuatilii maisha ya wapenzi wake wa zamani wala kujali  kuhusu wanawake watakaochumbia baada yake.

•Mobetto aliweka wazi kwamba hajutii ya kale kwani alipokuwa kwenye mahusiano yale akili zake zilikuwa timamu.

Hamisa Mobetto na Diamond Platnumz
Hamisa Mobetto na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM

Mwigizaji maarufu Bongo Hamisa Mobetto amepuuzilia mbali madai kwamba amekuwa akionekana sana na watu mashuhuri duniani kwa sababu anajaribu kumkomoa aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz.

Akiwa kwenye mahojiano na wanahabari, Mobetto aliweka wazi kwamba kwa kawaida yeye  huwa hana matatizo yoyote na mpenzi wake yeyote wa zamani .

Mama huyo wa watoto wawili alisema huwa hafuatilii maisha ya wapenzi wake wa zamani wala kujali  kuhusu wanawake watakaochumbia baada yake. Alisema huwa hana kinyongo chochote dhidi ya mpenzi wake yeyote wa zamani.

"Mimi ni mpenzi wa zamani asiye na matatizo. Mimi ni Ex ambaye siwezi kujali kuhusu kile unachofanya sasa hivi. Huwa najali cha kwangu kwa muda wangu. Ikitokea kwamba tumeachana, hayo yameisha. Siwezi kujali ukiwa na mwanamke mwingine na sidhani kama nimewahi kujali kwa Ex wangu yeyote akiwa na mwanamke mwingine. Naamini kwamba kila kitu kinatokea kwa sababu ni chema, kitu kikija kwako ni cha kwako. Kama sio cha kwako basi sio cha kwako. Pia naamini watu huchumbiana na kuachana, mkiachana inamaanisha riziki inaishia hapo ama Mwenyezi Mungu alitaka ufike hapo uendelee na safari. Mimi sijawahi wazia ex wangu yeyote yule vibaya. Sijawahi kufanya kitu kwa ajili ya yeyote yule. Huwa nafanya mambo yangu, na kufanya yale yanayonifurahisha" Alisema Mobetto.

Mwigizaji huyo ambaye amewahi kuwa kwenye mahusiano na watu wawili mashuhuri Bongo, Diamond na mfanyibiashara Francis Ciza Majizzo alisema hajutii kuwahi kuchumbia mpenzi wake yeyote wa zamani.

Mobetto aliweka wazi kwamba hajutii ya kale kwani alipokuwa kwenye mahusiano yale akili zake zilikuwa timamu.

"Huwa sijutii vitu. Borake nilipokuwa nafanya vile nilikuwa na akili zangu zote timamu  basi sijutiii. Huwa naamini pia kuwa  kila kitu kinatokea kwa sababu zake" Alisema.

Hivi majuzi uvumi ulitanda kote mitandaoni kwamba huenda mwigizaji huyo alikuwa ameingia kwenye mahusiano na rapa Rick Ross baada yao kuonekana wakijiburudisha pamoja Dubai.

Mobetto alisema kando na Rick Ross pia anafahamiana na watu wengine wengi mashuhuri duniani ambao huwa anawasiliana nao mara kwa mara