"Najiona kama sijawahi kuwa na Ex!" Jacque Wolper azungumzia mahusiano yake na mpenziwe Rich Mitindo

Muhtasari

•Wolper alisema mpenzi wake amemmininia mapenzi kochokocho kiasi cha kwamba amesahau mahusiano yake yote yaliyopita.

•Alisema ingawa yeye ni mwanamke mwenye wivu huwa hamchunguzi sana mpenziwe kwa kuwa anamwamini  sana na hajawahi kuona vikwazo vivyote vya kumshinikiza amchunguze.

•Alikiri kwamba hapo awali amewahi kuwa kwenye mahusiano na watu wenye matatizo ila akasema yeye mwenyewe hajawahi kuwa na tatizo lolote katika mahusiano hayo.

Image: INSTAGRAM// RICH MITINDO

Aliyekuwa mpenzi wa Harmonize, mwigizaji Jacquline Wolper amefunguka kuhusu mahusiano yake na mpenzi wake wa sasa Rich Mitindo.

Akiwa kwenye mahojiano na wanahabari hivi majuzi, Wolper alikiri anafurahia sana mahusiano yake ya sasa na kuweka wazi kuwa anamwamini baba ya mtoto wake sana.

Wolper alisema mpenzi wake amemmininia mapenzi kochokocho kiasi cha kwamba amesahau mahusiano yake yote yaliyopita.

"Mimi kusema kweli sikumbuki mambo ya zamani. Najiona kama kwamba sijawahi kuwa na Ex. Nina raha sana. Yaani kuna muda unafurahia hadi unajiona kama huna Ex, ndio mimi yaani. Penzi letu liko kwenye eneo" Wolper alisema.

Wolper alimlimbikizia sifa tele mpenzi wake Mitindo na kumtaja kama mpenzi bora kupitiliza na asiye na doa lolote.

Alisema ingawa yeye ni mwanamke mwenye wivu huwa hamchunguzi sana mpenziwe kwa kuwa anamwamini  sana na hajawahi kuona vikwazo vivyote vya kumshinikiza amchunguze.

"Mimi nina wivu. Kwa kweli mtu anayependa mwingine lazima ana wivu. Mwanamke ambaye ni mwaminifu ana wivu sana. Nina wivu mno ila lazima uamini mwenzio. Kama anakuheshimu lazima umwamini. Ikitokea jambo labda ndio nitataka kuingia kwenye simu ya mwenzangu. Tayari ananionyesha uaminifu sana. Sipati sana muda wa kuchunguza kwa sababu tayari sioni vikwazo. Endapo nitaona vikwazo kwa kweli nitamchunguza kila siku... Tayari naona ata kumkuta na kosa litakuwa kosa la kutafuta na tochi lakini sio kosa la wazi. Sijawahi kukutana na kosa lolote" Wolper alisema.

Wolper alisema huwa hana muda wa kujadili mahusiano yake ama mume wake na watu wengine wala kusikiliza maneno ya watu dhidi yake.

Alisema katika kipindi ambacho amechumbia Mitindo  hajawahi  kutamani tena maisha ya pekee kwa kuwa anafurahia  sana mahusiano yao.

"Sijawahi kutamani kuwa singel wala sijawahi kutamani kuachana naye kwa sababu kwangu mimi yeye ni mtu aliyepitiliza.. Vikwazo vipo, lakini vya kawaida tu" Alisema.

Mwigizaji huyo alikiri kwamba hapo awali amewahi kuwa kwenye mahusiano na watu wenye matatizo ila akasema yeye mwenyewe hajawahi kuwa na tatizo lolote katika mahusiano hayo.