Je, Hamisa Mobetto kateka moyo wa Rick Ross? Matendo yake ya hivi majuzi mtandaoni yazua gumzo

Muhtasari

•Ujumbe wa hivi majuzi wa Mobetto kwenye ukurasa wake wa Instagram ambao inaaminika alikuwa anazungumzia Rick Ross umeibua uvumi zaidi kuhusu mahusiano yao.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Mwanamitindo na mwanamuiziki mashuhuri kutoka Bongo Hamissa Mobetto ameendelea kudokeza kwamba huenda amepata kipenzi kipya.

Matendo ya mpenzi huyo wa zamani wa Diamond  Platnumz ya hivi majuzi mitandaoni yameendelea kuashiria huenda ni kweli amejitosa kwenye mahusiano ya kimapenzi na rapa Rick Ross kutoka marekani.

Ujumbe wa hivi majuzi wa Mobetto kwenye ukurasa wake wa Instagram ambao inaaminika alikuwa anazungumzia Rick Ross umeibua uvumi zaidi kuhusu mahusiano yao.

"Inachukua mwanaume wa kweli kutengeneza moyo ambao hakuuvunja na kulea mtoto ambaye hakumpata" Mobetto aliandika.

Haya yanajiri takriban wiki tatu baada ya Mobetto na Rick Ross kuonekena pamoja jijini Dubai katika hali iliyoibua maswali mengi mitandaoni.

Kwenye video na picha ambazo walipakia mitandaoni, wawili hao walionekana wakijiburudisha pamoja katika maeneo mbalimbali ya burudani jijini humo kama wapenzi.

Mobetto alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na rapa huyo alisema ni kama wa 'kifamilia' kwani wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa muda.

Mobetto hakukiri uwepo wa mahusiano ya kimapenzi kati yake na rapa huyo wala kukana huku akiahidi kufahamisha watu hivi karibuni iwapo kuna chochote cha ziada kati yao.

"Mimi na Ross ni familia. Saa hii tumekuwa familia, hayo ndiyo naweza kusema. Zaidi ya hayo mimi nimekuwa balozi wa Belaire hapa Tanzania. Huwa tunafanya kazi pamoja... Kama kutakuwa na kitu chochote kitatokea mtajua tu" Alisema Mobetto.

Mobetto alisema ziara yake ya Dubai ilikuwa ya kikazi tu ikiwemo kujadiliana na Rick Ross ambaye ni mshirika wake kazini.

Mwanamuziki huyo wa Bongo alitengana na Diamond Platnumz zaidi ya miaka mitano iliyopita baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa muda na kubarikiwa na mtoto mmoja.