Msanii wa Bongo Marioo amekiri kuwa aliumia sana moyoni baada ya kutazama video ya mpenzi wake akiogelea kwenye bwawa la mwanamuziki mwenzake Diamond Platnumz.
Mwaka wa 2020 Mimi Mars alionekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni akiogelea kwenye bwawa moja na Diamond.
Baada ya video hiyo kusambaa kote mitandaoni uvumi ulitanda kuwa wawili hao wapo kwenye mahusiano ya kimapenzi.
Marioo akishirikisha mashabiki wake kwenye kipindi cha maswali na majibu amefichua kuwa hilo ndilo tukio ambalo limewahi kuumiza zaidi maishani.
"Yapo mengi ila nilivoonaga ile klipu video ya rafiki yangu wa kike anaogelea kwenye pool la broo ilinigusa nayo ile," Marioo alimjibu shabiki aliyeuliza kuhusu tukio ambalo limewahi kumuumiza zaidi.
Kwenye video hiyo Diamond na Mimi Mars walionekana ndani ya maji wakiwa wamevalia mavazi ya kuogelea huku wakijivinjari na kucheka.
Hapo awali Diamond alikuwa amepakia video ya Mars ambaye ni dada ya Vanessa Mdee akinengua kiuno kwa wimbo wake 'Cheche'.
“Mi nakapendaga haka katoto…. Sema sjui ata Tyming naikoseaga wapi Mwana wa Dangote… Doh! @mimi_mvrs11 ….. #CHECHE,” Diamond aliandika chini ya video hiyo.
Baadae hata hivyo Mars alijitokeza kupuuzilia mbali madai kuwa yupo kwenye mahusiano na bosi huyo wa Wasafi.
Licha ya yaliyotokea ni wazi kuwa hakuna uhasama wowote kati ya mwanamuziki huyo na Diamond kwa kuwa hata wanapanga kuachia colabbo pamoja hivi karibuni.