Mwanamuziki wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ni miongoni mwa wasanii ambao wamechorwa tattoo nyingi kwenye mwili wao.
Harmonize amechorwa tattoo zaidi ya kumi kwenye mikono, miguu, shingo, kifua, mgongo na kiuno chake. Baadhi ya tattoo zake ni michoro huku zingine zikiwa maandishi.
Tattoo nyingi za bosi huyo wa Konde Music World huwa na maana zake tofauti huku baadhi zikiwa za kusherehekea watu maalum katika maisha yake.
Katika makala haya tutaangazia baadhi ya tattoo za msanii huyo na maana yake;-
1. Tattoo ya Diamond
Miaka kadhaa iliyopita Harmonize alichorwa sura ya aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz kwenye kifundo cha mkono wake kushoto.
Mwaka jana mwanamuziki huyo alithibitisha kuwa tattoo hiyo bado ipo licha ya uhasama mkubwa uliopo kati yao.
"Licha ya yote, mimi nina heshima kubwa kwake. Leo hii licha ya makelele yote unayosikia niko na tatoo ya Diamond. Hii ni sura yake. Licha ya yote!" Harmonize alisema.
Konde Boy alisema alipokuwa anachora tattoo ile alitaka iwe kumbukumbu kuwa Diamond alimuinua kutoka sehemu moja hadi nyingine.
2. Tattoo ya jina lake
Mwanamuziki huyo kutoka eneo la Mtwara amechorwa tattoo ya jina lake la utani "Konde Boy" kwenye mkono wake wa kulia.
Tattoo hiyo ni maalum kwake kwa kuwa ni ishara ya kujipenda.
3. Tattoo ya Sarah Michelloti
Mwaka wa 2019 Harmonize alichora tattoo ya jina la aliyekuwa mpenzi wake Sarah Michelloti kwenye mkono wake.
Mwanamuziki huyo alipiga hatua hiyo wakati penzi lake na Sarah lilikuwa limenoga kama ishara ya kumsherehekea kipusa huyo.
Wawili hao hata hivo walitengana baada ya Harmonize kufichua habari kuhusu mtoto ambaye alipata nje ya ndoa.
4. Tattoo ya Kajala na bintiye
Mapema mwaka huu, hatua ya Harmonize kuchorwa tattoo ya aliyekuwa mchumba wake Fridah Kajala Masanja imekuwa gumzo kubwa mitandaoni.
Jambo hili lilifichuka baada ya mwanamuziki huyo kupakia video iliyoonyesha tattoo ya sura ya muigizaji huyo akiwa amemshika binti yake Paula.
Harmonize alipiga hatua hiyo kama mojawapo ya njia ya kumtongoza Kajala ili warudiane tena baada ya kuwa wamekosana mwaka jana.
5. Tattoo ya Magufuli
Mwaka jana Harmonize alichorwa tattoo ya sura ya rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, John Pombe Magufuli.
Harmonize alichorwa tattoo hiyo baada ya hayati kufariki kama hatua ya kusherehekea maisha yake.