Muigizaji na mwanamuziki maarufu Wema Sepetu ameweka wazi kwamba yupo tayari kushirikiana na aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz katika kazi ya usanii.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akizinduliwa kama balozi mpya wa Kodtec, Wema alifichua kwamba kwanza anakusudia kumualika Diamond katika shoo yake ya Cook with Wema.
Wema alitumia fursa hiyo kumuomba mpenzi huyo wake wa zamani kukubali mwaliko katika kipindi chake wakati huo utakapofika.
"Bwana Simba nitakapokuja kukuomba ushiriki katika kipindi changu basi naomba unipokee kwa mikono miwili. Nina imani tutafanya kipindi ambacho kitakuwa kizuri sana ambacho hakijawahi kutokea tangu Cook with Wema ilipoanza," Wema alisema.
Alisema kwamba yeye yupo tayari kabisa kuwa na kikao na bosi huyo wa WCB huku akiweka wazi kwamba hatamlazimisha kushiriki.
"Akinikatalia nitamshtaki kwa wananchi ili mnisaidie kumuomba. Kuhusu mradi wetu wa Temptations kwa sababu hapa katikati kumetokea vitu vingi, sijui, mimi niko tayari kabisa kufanya kazi na mwenzangu. Sasa inategemea na yeye, inahitaji pande zote ziingiane na ziwe tayari. Mimi mwenyewe niko tayari , kama mwenzangu pia yupo tayari mbona isifanyike. Lengo ni kutumbuiza watu tu" Alisema.
Wema alifichua kuwa hapo awali amewahi kufanya muziki pamoja na mpenzi huyo wake wa zamani akiwa msanii wa kuingiza sauti. Alifichua kuwa Diamond alimshirikisha katika nyimbo zake 'Lala Salama' na 'Chanda Chema.'
Muigizaji huyo pia amefichua huenda akamtambulisha mpenzi wake wa sasa kupitia shoo yake ya Upishi katika siku zijazo.
"Namuachia Mungu kwenye hili. Anaweza akakubali ama akakataa. Anaweza kwa wakati huo akakuwepo ama akakosekana. Lakini natazamia sana kumtambulisha. Hapo baadae tutajua itakavyofanyika," Alisema.