Aliyekuwa mpenzi wa mwanasoshalaiti Amber Ray, Kennedy Rapudo amethibitisha kutengana kwao baada ya mahusiano ya kipindi kifupi.
Katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram, Rapudo alidokeza kuwa mahusiano yao yaligonga ukuta kutokana na tofauti za kimuundo zisizoweza kusuluhishwa.
Mfanyibiashara huyo hata hivyo aliweka wazi kuwa hana kinyongo chochote dhidi ya Amber Ray na kumtakia heri maishani.
"Ni mtu mzuri sana mwenye moyo wa ajabu na roho nzuri. Yangu ni kumtakia furaha na neema ya Mungu popote aendapo," Rapudo alisema.
Rapudo alisema alimpenda sana mwanasoshalaiti huyo wakati walipokuwa kwenye mahusiano na kubainisha kuwa walifaana.
"Yeye pia ni mkomavu na wa kifahari. Achana na yale mnayoyaona kwenye mitandao ya kijamii," Alisema.
Aidha aliweka wazi kuwa mama huyo wa kijana mmoja alikuwa mtiifu na mwaminifu sana walipokuwa wanachumbiana.
"Nilitoa yote yangu na kuweka mguu wangu bora mbele. Ninapoingia kwenye mahusiano, nipo ndani. Lakini kama nilivyosema, tulikuwa na tofauti zetu na nadhani sote tuko sawa na uamuzi wa mwisho," Alisema.
Baba huyo wa watoto wawili alifichua kuwa yeye na Amber Ray walitengana kwa ajili ya kutafuta uzoefu mpya.
Rapudo alisema kuwa kwa sasa yupo single na kubainisha kuwa hayupo tayari kujitosa kwenye mahusiano mapya.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Amber Ray kutangaza kutengana na Rapudo baada ya kipindi kifupi tu cha mahusiano.
Mwanasoshalaiti huyo aliweka wazi kuwa mahusiano hayo yalikataa kufaulu licha ya juhudi zote walizotia.
“Najua mahali imefika naweza kuonekana mcheshi lakini manze sijui nifanyeje kama haifanyi kazi.....haifanyiki...so munipende tu vile niko,” Amber Ray alisema kwenye Instagram.
Wawili hao walianza kuchumbiana takriban miezi miwili iliyopita baada ya Amber Ray kuachana na mchezaji mpira wa vikapuwa Sierra Leone, IB Kabba.