Siku ya Jumatano wanandoa mashuhuri kutoka Bongo Bilnass na Nandy walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza pamoja.
Wasanii hao wawili ambao walifunga pingu za maisha mwezi Julai walitangaza ujio wa binti yao kupitia mitandao ya kijamii.
Nandy alisherehekea kujifungua kwa mafanikio na kumshukuru mumewe kwa kumfanya aweze kukutana na uzao wake.
"Ninachoweza kusema ni NAKUPENDA SANA MAMA maana nimeona umuhimu na ugumu wa kukamilisha kuitwa MAMA, nyie na furaha sijawahi kupata maishani mwangu nilijua nimefurahi na mengi lakini kumbe bado,,,!!! hii ni furaha ya kweli toka moyoni❤️," Nandy alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Malkia huyo wa Bongo alimtaja bintiye kuwa rafiki wake wa dhati.
Kwa upande wake Bilnass alisema 2022 umekuwa mwaka wa baraka sana maishani mwake. Huu ndio mwaka aliofunga ndoa na kubarikiwa na mtoto.
Rapa huyo alitoa shukrani kemkem kwa mkewe Nandy na kumtambua kuwa shujaa kwa ujasiri aliouonyesha wakati wa ujauzito na kujifungua.
"Haikuwa Kazi Rahisi umenionesha wewe ni Shujaa kiasi gani kwanzia Mtoto akiwa tumboni mpaka Muda unajifungua umepigana sana. Nimejionea namna gani mtu anaweza ku risk kupoteza uhai wake wakati wa kujifungua," Alisema.
Bilnass alibainisha kuwa kipindi cha ujauzito na kujifungua kwa mkewe kimefanya upendo wake kwake kukua zaidi.
Kufuatia hayo, rapa huyo alimuahidi Nandy upendo na amani tele katika maisha yao ya ndoa na kumuombea ulinzi wa Mungu.
"Nikuhakikishe uko Mikono Salama 🙏🏿🙏🏿🙏🏿 !!" Alimwambia mkewe.
Bilnass alisema kuzaliwa kwa bintiye kumewaletea baraka tele. Pia alimhakikishia mtoto huyo wake kuhusu upendo wake mkubwa kwake.
"Mwenyezi Mungu akutunze kwa Mapenzi yake na Ukawe mtu mwema katika ulimwengu wa kawaida na wa kiroho," Alisema rapa huyo.
Katika mahojiano ya awali, nandy aliweka wazi kuwa makubaliano yake na mumewe ni kwamba hakuna kutaja jina la mtoto wao wala kuonesha sura yake na hata kumfungulia akaunti za mitandaoni.
“Sidhani kama tutaliweka wazi jina la mtoto wala sidhani kama tutakuja kutoa jinsia yake au hata kuwa na ukurasa wake wa Instagram wala kuonekana hata kidogo mitandaoni,” alisema Nandy wakati hafla ya Nandy Festival.
Msanii huyo alieleza kwamba waliamua vile ili kumpa mtoto wao nafasi ya kukua mwenyewe ili akishafikisha umri wa kujielewa basi akajifanyie mambo hayo mwenyewe.